Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 07:48

Burundi : Mwendesha mashtaka aitaka mahakama itoe adhabu ya miaka 15 kwa waandishi 4


Wanahabari Christine Kamikazi, Agnes Ndirubusa, Egide Harerimana, Terence Mpozenzi
Wanahabari Christine Kamikazi, Agnes Ndirubusa, Egide Harerimana, Terence Mpozenzi

Mwendesha mashtaka wa Burundi Jumatatu ameomba mahakama itoe adhabu ya kifungo cha miaka 15 kwa wanahabari wanne wa gazeti la Iwacu linalo chapisha habari zake kupitia mtandao wa intanet.

Katika kesi iliyo sikilizwa na mahakama ya mkoa wa Bubanza, kaskazini magharibi mwa Burundi, mwendesha mashtaka huyo amewashtumu wanahabari hao kwa kushirikiana na kundi la waasi lililofanya shambulizi katika mkoa huo mwezi Oktoba.

Lakini wanahabari hao wamepinga shutuma hizo, wakisema walikuwa wanafanya kazi yao ya kuchunguza habari wakati lilipotokea shambulizi hilo.

Mawakili wao wameiomba mahakama kuwaachia huru wateja wao, wakieleza kuwa wanahabari hao walitekeleza wajibu wao wa kuwajuza wananchi kuhusu yaliyo kuwa yanaendelea nchini. Uamzi wa mahakama unasubiriwa kutolewa katika kipindi cha siku 30 zijazo.

Wanahabari Christine Kamikazi, Agnes Ndirubusa, Egide Harerimana, Terence Mpozenzi na dereva wao walikamatwa tarehe 22 Oktoba, 2019, katika mkoa huo wa Bubanza. Dereva wao aliachiwa baadae kwa dhamana.

Burundi imekuwa ikishutumiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu kwamba inakandamiza uhuru wa uandishi wa habari na uhuru wa kutoa maoni.

Mwezi Machi 2019, serikali ya Burundi ilipiga marufuku radio ya Uingereza BBC kutoa tena matangazo yake nchini humo, sauti ya Amerika VOA nayo ilisimamishwa kuendelea na shughuli zake kwa muda usiojulikana kikomo chake.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG