Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 21:08

Bunge Kenya lawapitisha mawaziri wote 24 walioteuliwa na Rais Ruto


Ruto
Ruto

Bunge la Kenya Jumatano hatimaye limeidhinisha uteuzi wa mawaziri wote 24 kuhudumu kwenye baraza la mawaziri la rais William Ruto.

Bunge la Kenya Jumatano hatimaye limeidhinisha uteuzi wa mawaziri wote 24 kuhudumu kwenye baraza la mawaziri la rais William Ruto.

Katika orodha hiyo yupo Waziri mteule wa Utalii Penina Malonza, ambaye awali Kamati ya Uteuzi ilimkataa kwa kukosa uwezo na uzoefu wa kitaaluma unaohitajika.

Licha ya kuwepo pingamizi inayotokana na mashaka ya uadilifu, bunge hilo pia limeidhinisha uteuzi wa Aisha Jumwa kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma na Jinsia pamoja na Mithika Linturi kuwa Waziri wa Kilimo.

Mchakato wa uteuzi wa maafisa 24 kwenye baraza la mawaziri la utawala wa rais William Ruto, umekamilika Jumatano ili kupisha uapisho wakati wowote sasa.

Hii ni kufuatia bunge hilo kuidhinisha ripoti ya kamati ya uteuzi uliofanyiwa marekebisho madogo kuruhusu uidhinishaji wa Waziri mteule wa Wizara ya Utalii na Turathi za Kitaifa Penina Malonza aliyekuwa ametemwa nje kwa kukosa uwezo na uzoefu wa kitaaluma unaohitajika kusimamia wizara hiyo.

Wabunge wakiwa katika kikao ndani ya jengo la Bunge la KenyaParliament Nairobi, June 10, 2021.
Wabunge wakiwa katika kikao ndani ya jengo la Bunge la KenyaParliament Nairobi, June 10, 2021.

Licha ya Malonza kuafiki vipimo vya uadilifu, uaminifu, na mienendo yake, inavyohitajika katika utumishi wa umma, kamati hiyo, katika ripoti yake, iliyoidhinisha kwa kauli moja, ilieleza kutoridhishwa na uwezo na uzoefu wake kuwa waziri.

Ingawa wanakamati wote walikubaliana kuwa Malonza "hakuonyesha ujuzi juu ya masuala ya mada, utawala na kiufundi yanayogusa Wizara ya Utalii" hivyo basi hawezi kuidhinishwa kuwa sehemu ya baraza la mawaziri la Bw Ruto.

Pia wabunge kwa kauli moja walitupilia mbali mapendekezo ya ripoti hiyo kwa kuyataja kuwa yasiyokuwa na uzito wa aina yoyote kumzuia Malonza kuwa Waziri wa Utalii na Turathi za Kitaifa, anaeleza Sarah Korere, Mbunge wa Laikipia Kaskazini.

Baadhi ya wabunge walieleza kuwa bunge hilo haliwezi kudhibiti uteuzi wa Malonza wakati wapo walioteuliwa wanaokabiliwa na shutuma za uhalifu na wameidhinishwa kwa kauli moja.

Mbunge wa Lugari Nabii Nabwera alionekana kughadhabishwa na jinsi Kamati hiyo ya Uteuzi ilivyozingatia vigezo vya kikatiba vilivyotumika kuwapiga msasa na kuwaidhinisha baadhi ya walioteuliwa na Rais Ruto.

Nabii Nabwera, Mbunge, Lugari anasema: Licha ya kuwapo pingamizi la chama cha Upinzani linatokana na mashaka ya uadilifu dhidi ya Aisha Jumwa kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma na Jinsia pamoja na Mithika Linturi kuwa Waziri wa Kilimo, bunge hilo limepuuza pingamizi hilo na kuwaidhinisha pia.

Wabunge wanane kwenye kamati hiyo ya uteuzi walikuwa wameandika ripoti mbadala inayopendekeza kukataliwa kwa uteuzi wa Mithika Linturi na Aisha Jumwa, kwa misingi kuwa hawaafiki vipimo vya uadilifu kwa mujibu wa Ibara ya 232 ya katiba, inayohitaji mawaziri kuwa na maadili na viwango vya juu vya kitaaluma, na uwajibikaji.

Bw Linturi alitiliwa shaka kutokana na kukiri kwake kuwa anaandamwa na msururu wa kesi 35 mahakamani ambazo wabunge walieleza kuwa huenda zikaathiri utendaji kazi wake.

Pia, wabunge hao walitaka Bw Linturi kukataliwa kwa kushindwa kuwasilisha nakala ya shahada ya kitaaluma ambayo anasema aliipata kutoka Chuo Kikuu cha India.

Uteuzi wa Jumwa, kwa upande mwingine, ulipuuzwa kutokana na kesi iliyokuwa ikiendelea mahakamani ambapo anadaiwa kumpiga risasi mwanamume mmoja mwaka 2019 wakati wa uchaguzi mdogo wa Wadi ya Ganda, eneo bunge la Kilifi.

Aisha Jumwa
Aisha Jumwa

Richard Bosire, Mfuatiliaji wa siasa za Kenya anaeleza kuwa kupitishwa kwa maafisa hao ni afueni kubwa kwa Bw Ruto.

Wabunge walioteuliwa kuwa mawaziri kama vile Aden Duale, Waziri Mteule wa Ulinzi, Kipchumba Murkomen, Waziri Mteule wa Uchukuzi, na Alice Wahome, Waziri Mteule wa Maji, wamejiuzulu Jumatano kupisha uapisho wao wakati wowote na Rais Ruto.

Miongoni mwa nyadhifa mpya zilizoundwa kwenye baraza la Mawaziri la rais Ruto ni nafasi ya Mkuu wa Mawaziri inayosimamiwa na makamu wa rais wa zamani Musalia Mudavadi atakayekuwa na majukumu ya kumsaidia Ruto katika uratibu na usimamizi wa wizara na idara za serikali, pamoja na kusimamia utekelezaji wa sera, mipango na miradi ya serikali ya kitaifa, katika wizara zote.

Bw Mudavadi, ataongoza na kuratibu ajenda za sheria za serikali ya kitaifa katika wizara na idara zote za serikali kwa mashauriano na mawasiliano na uongozi wa bunge la Kenya pamoja na kuwezesha utekelezaji wa mipango ya wizara zote serikalini na kusimamia ufuatiliaji wa kiufundi na kutathmini utekelezaji wa sera, mipango na miradi ya serikali katika wizara zote, miongoni mwa majukumu mengine.

Imetayarishwa na mwandishi wetu KENNEDY WANDERA, NAIROBI.

Zinazohusiana

XS
SM
MD
LG