Tukio hili ni moja ya mauaji ya watu wengi yaliyo ripotiwa wakati wa mzozo uliozuka karibu miezi minne iliyopita katika mkoa wa kaskazini wa Tigray.
Katika kipindi cha takriban saa 24, tarehe 28-29 Novemba 2020, wanajeshi wa Eritrea wanaofanya operesheni katika mji wa Axum wa Ethiopia wanadaiwa waliwaua mamia ya raia, Amnesty ilisema, ikinukuu mashahidi 41.
Shirika hilo la haki lilisema kwamba kuuwawa kwa raia na wanajeshi wa Eritrea kunaweza kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Kikosi kazi cha dharura cha serikali ya Ethiopia kwa ajili ya Tigray kilisema Alhamisi kwamba uchunguzi wa ghasia huko Axum ulikuwa ukiendelea.
Tume ya Haki za Binadamu ya Ethiopia inayosimamiwa na serikali ilitoa taarifa iliyowekwa kwa wakati muafaka na ripoti ya Amnesty, ikisema kuwa uchunguzi wa awali ulionyesha kwamba wanajeshi wa Eritrea waliua idadi isiyojulikana ya raia huko Axum kwa kulipiza kisasi shambulio la hapo awali la wanajeshi wa Tigray -Tigray People's Liberation Front ( TPLF), chama tawala kilichotengwa katika mkoa huo.