Ofisi ya Hamdok imesema mkutano huo ulifanyika, pembeni ya mkutano wa viongozi wa Jumuia ya IGAD huko Djibouti. Taarifa inaeleza kwamba kufuatia mkutano huo maafisa wa Sudan na Ethiopia watakutana Jumanne mjini Khartoum mji mkuu wa Sudan kwa ajili ya mazungumzo kuhusiana na mzozo huo bila ya kutoa maelezo zaidi.
Mkutano wa viongozi hao wawili umefanyika siku chache baada ya mashambulizi ya kuvuka mpaka yaliyofanywa na wanajeshi wa Ethiopia na wanamgambo ambayo yaliuwa wanajeshi wa Sudan wasiopungua wanne na kujeruhi darzeni ya wengine katika eneo la Abu Tyour, katika jimbo la mashariki la Sudan la Qadarif.
Shirika la habari la serikali ya Sudan SUNA, limeripoti Jumamosi kuwa jeshi limepeleka “msaada mkubwa wa kijeshi” katika jimbo la al-Qadarif kurejesha maeneo yake yanayo shikiliwa na wakulima wa Ethiopia na wanamgambo katika eneo la mpakani la Al-Fashqa, Sudan. Wanajeshi hao wafika hadi eneo la mpakani lililokubaliwa kufautana na mkataba wa mwaka 1902 uliofikiwa kati ya Sudan na Ethiopia.
Mashambulizi ya kuvuka mpaka yaliyofanyika Jumanne katika eneo la Abu Tyour yamefanyika wakati kumekuwepo mapigano ya wiki nzima katika jimbo la kaskazini mwa Ethiopia la Tigray, ambako wakuu wa jimbo wakipinga mamlaka ya serikali kuu.
Mapigano ya Tigray yamesababisha zaidi ya wakimbizi wa Ethiopia 52,000 kukimbilia Sudan, wengi wao wakiwasili katika jimbo la al-Qadarif.