Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 19:06

UNHCR yaomba kuingia kwenye kambi za wakimbizi huko Tigray


Wakimbizi wa Eritrea wakingoja kuingia katika kambi ya Indabaguna katika mkoa wa Tigrai February 9, 2016.
Wakimbizi wa Eritrea wakingoja kuingia katika kambi ya Indabaguna katika mkoa wa Tigrai February 9, 2016.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi linatoa wito kwa viongozi wa serikali ya Ethiopia kutoa fursa ya kufika kwenye kambi zinazowahifadhi maelfu ya wakimbizi wa Eritrea ambao wamekuwa hawana msaada wa kibinadamu tangu kuanza kwa mzozo katika mkoa wa Tigray nchini Ethiopia mapema mwezi uliopita

Chakula mara ya mwisho kugawiwa katika kambi hizo kwa ajili ya wakimbizi 96,000 wanaopatiwa makazi katika kambi nne ni kabla ya jeshi la Ethiopia kuanza mashambulizi ya kijeshi kwa Tigray Novemba 4.

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa linasema kwa sasa kambi hizo zimeishiwa na vyakula, na kufanya njaa na utapiamlo kuwa ni hatari ya kweli. Pia inaelezea wasiwasi juu ya usalama wa wakimbizi, ambao wengi wao wanaweza kuwa katika hatari ya kuwa katika eneo la mashambulizi.

Msemaji wa UNHCR Babar Baloch anasema haiwezekani kuthibitisha kile kinachotokea kwa sababu mawasiliano yote huko Tigray yamekatwa; lakini, anasema kuna ripoti kwamba baadhi ya wakimbizi huenda wamekimbia kutoka katika kambi na sasa ni wakimbizi wa ndani katika eneo la kaskazini mwa Ethiopia.

“Na wakimbizi wengine ambao wako kwenye kambi, huenda wakaanza kuhama pia. Lakini kwa upande wa mashambulizi, utekaji nyara, uandikishaji wa lazima, hizi zote ni ripoti zenye kutia wasiwasi ambazo zimetufikia. Kwa hivyo, wakati ambapo hatuwezi kufika ni ngumu sana kuthibitisha.”

Baloch anasema ni muhimu kwamba watoa misaada ya kibinadamu waruhusiwe kufikia na kusaidia watu hawa wanaohitaji misaada sana.

Wakati huo huo, UNHCR inaripoti Waethiopia wanaendelea kukimbilia Sudan kutafuta usalama. Inasema karibu watu 46,000 sasa wamewasili. Baloch, hata hivyo, anabainisha kuwa idadi inayofika kila siku sasa imepungua kutoka maelfu hadi mamia.

“Wakimbizi hao ambao wanafika sasa, wanataja kuona vituo zaidi vya ukaguzi kwenye barabara ambazo zinaunganisha Ethiopia na Sudan. Wanataja ugumu wa kuzunguka, kwa hivyo lazima wachukue njia nyingine kufika Sudan.” alisema Baloch.

UNHCR inasema watu wanaotafuta usalama na misaada hawapaswi kuzuiwa kufanya hivyo iwe ndani ya nchi yao au katika mipaka ya kimataifa. Shirika hilo linaomba dola milioni 147 kutoa msaada wa kibinadamu kwa wakimbizi hadi 100,000 kwa miezi sita ijayo.

Imetayarishwa na Sunday Shomari, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG