Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 14:55

Mamilioni ya Watoto hawapati msaada muhimu Tigray, Ethiopia kutokana na vita eneo hilo


Umoja wa mataifa umeonya kwamba mamilioni ya Watoto katika eneo la Tigray nchini Ethiopia hawawezi kufikiwa, licha ya kuwepo mkataba uliosainiwa mapema mwezi huu kuhakikisha kwamba msaada wa kibinadamu unaohitajika zaidi kaskazini mwa eneo hilo unawafikia watu.

Mapigano ya mwezi mzima yameua watu kadhaa, kujeruhi na kusababisha maelfu ya watu kuachwa bila makao.

Mkurugenzi wa shirika la umoja wa mataifa la kuwashughulikia Watoto UNICEF, Henrietta Fore, amesema kwamba karibu Watoto milioni 2.3 katika eneo la Tigray hawawezi kufikiwa kwa ajili ya kupewa msaada wa kibinadamu.

Makubaliano kati ya umoja wa mataifa na serikali ya Ethiopia, yaliyotangazwa Desemba tarehe 2, yalilenga kuhakikisha kwamba wafanyakazi wa kutoa msaada wanaingia katika eneo linalodhibitiwa na serikali katika sehemu za Tigray, ambapo wanajeshi wa serikali wamekuwa wakipigana na vikosi vya Tigray TPLF.

Vita vya Tigray vinaaminika kusababisha vifo vya maelfu ya watu, 45,000 kukimbilia Sudan kama wakimbizi na kuacha wengi kadhaa bila makao ndani ya Tigray.

Zaidi ya watu 600,000 walikuwa wanategemea msaada wa chakula hata kabla ya vita hivyo.

Maafisa wa UNICEF wamesema kwamba hali imeendelea kuwa ngumu kwao kufikisha msaada wa kibinadamu katika eneo hilo licha ya kusainiwa makubaliano ya kuwaruhusu kufanya hivyo.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG