Waziri Kabudi awaonya wenye kuisema vibaya Tanzania

Waziri Palamagamba Kabudi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Palamagamba Kabudi, Jumatatu, amewaonya wale wote wanaojaribu kuisema vibaya Tanzania.

Kabudi amesisitiza kuwa : “Huu siyo wakati wa kuisema vibaya nchi yetu, huu siyo wakati wa kuibagaza nchi yetu, huu siyo wakati wa kuibeza nchi yetu.”

Kabudi wakati akipokea jukumu la wizara hiyo baada ya kuapishwa na Rais John Magufuli aliwakumbusha wananchi kuwa "Tanzania iliyojengwa na huyo ambaye sura yake inatuangalia (Mwalimu Julius Kambarage Nyerere) kuwa siyo nchi ya kuchezewa."

Akionyesha kukerwa na vitendo hivyo ya kuisema vibaya Tanzania, mbele ya Rais Magufuli alieleza :“Tanzania siyo nchi ya kudharauliwa, siyo nchi ya kudhihakiwa. Na yeyote Mtanzania ambaye ana matatizo na nchi hii atutendee jambo moja tu, akae kimya, akae kimya. Kama imemshinda kutosema yasiyofaa kwa nchi yake.”

Kabudi amesema watanzania wanajukumu moja kubwa sasa, la kuijenga nchi yetu na kuimarisha uhusiano na urafiki na wale wote wanaotutakia mema na wote wanakaribishwa katika nchi hii ili kwa pamoja tufanye yaliyo bora , ili nchi yetu isonge mbele.

Ameongeza kuwa : "Tushirikiane ili nchi yetu ipate maendeleo na wananchi wetu wapate yale wanayoyahitaji.

Rais Magufuli wiki hii alifanya mabadiliko madogo katika baraza lake la mawaziri kwa kumteua Dkt Augustine Mahiga kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Dkt Mahiga amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki tangu Desemba 10, 2015, wakati Rais Magufuli alipotangaza baraza la kwanza la mawaziri baada ya kuingia madarakani Novemba 5, 2015.

Profesa Kabudi kwa upande wake, amekuwa Waziri wa Katiba na Sheria tangu Machi 23, 2017 baada ya Rais kufanya mabadiliko akichukua nafasi ya Dk. Harrison Mwakyembe aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Aidha, mabadiliko ya jana yalifanyika ikiwa takriban miezi mitatu tangu Novemba 23, mwaka jana wakati Rais Magufuli alipofanya mabadiliko kama hayo.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Washington, DC.