Watu saba wapoteza maisha karibu na uwanja wa ndege wa Kabul

Watoto waliokuwa tayari kuondolewa Afghanistan wakisubiri ndege ya pili baada ya majina yao kuorodheshwa kama wasafiri halali katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Hamid Karzai, Kabul, Afghanistan, Agosti 19, 2021. Photo by Mark ANDRIES / US MARINE CORPS / AFP)

Watu saba wameuawa karibu na uwanja wa ndege wa Kabul Jumamosi wakati maelfu walipokusanyika katika hali ya kukata tamaa wakihangaika kuondoka nchini huku Taliban wakidhibiti maeneo mbalimbali, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imesema Jumapili.

Taliban, baada siku 10 za mashambulizi, waliingia mji mkuu wa Afghanistan kiasi cha wiki moja iliyopita, Agosti 15.

Tangu wakati huo, uwanja wa ndege umekuwa eneo lenye vurugu huku maelfu ya watu wakijaribu kuondoka nchini, wakihofia kurejea kwa tafsiri kali ya sheria ya Kiislam iliyotumika wakati Taliban walipokuwa wanatawala nchi hiyo miaka 20 iliyopita.

Raia wa Marekani wakipanda katika ndege za jeshi la Marekani.

“Mambo kadhaa bado yana changamoto kubwa huko lakini tunafanya kila tunaloweza kukabiliana na hali hiyo kwa njia ya usalama na utulivu kadiri inavyowezekana,” Wizara ya Ulinzi ya Uingereza amesema katika taarifa yake.

Viwango vya juu vya joto siku ya Jumamosi mjini Kabul vilifikia nyuzi joto Celsius 34. Shirika la Habari la Associated Press limeripoti kuwa haikuweza kufahamika mara moja iwapo waliokufa walikuwa wamekanyagwa, walikosa pumzi au walipata mshtuko wa moyo katika msongamano wa watu.

Mwandishi wa Kituo cha televisheni cha Sky News ambaye alikuwa katika uwanja wa ndege wa Kabul, hata hivyo, amesema maelfu ya raia wa Afghanistan walijitokeza Jumamosi pamoja na wale walioko mbele wakijaribu kutumia nguvu kuvuka vizuizi, Reuters imeripoti.

Pia siku ya Jumamosi, raia wa Marekani nchini Afghanistan wanaotaka kuondoka nchini wameshauriwa wasiende uwanja wa ndege wa Kabul ila tu kama wamepokea maelekezo binafsi kutoka kwa mwakilishi wa serikali ya Marekani kufanya hivyo.

Tahadhari ya usalama kutoka Ubalozi wa Marekani nchini Afghanistan inaonekana iliuongeza wasiwasi na taharuki wakati maelfu ya watu walioizunguka uwanja wa ndege wa Kabul wakitegemea kupata usafiri kuondoka tangu Taliban ilipochukua mamlaka nchini humo.

Rais Joe Biden

Rais wa Marekani Joe Biden amepangiwa kutoa habari za matukio mapya Jumapili mchana kuhusu kuondolewa kwa Wamarekani na wakimbizi wa Afghanistan kutoka Kabul.

Jumapili, Uhispania imetangaza kuwa itawapokea wakimbizi wa Afghanistan ambao walikuwa wakifanya kazi na serikali ya Marekani.

Raia wa Afghanistan watapatiwa hifadhi katika vituo viwili vya kijeshi kusini mwa Spain, Moron de la Frontera karibu na Seville na Rota karibu na Cadiz, wakati wakisubiri kusafirishwa kwenda katika nchi nyingine.