Stefano Pontecorvo, mwakilishi mwandamizi wa kiraia kwenye ushirika wa NATO nchini Afghanistan, alituma picha kupitia mtandao wa Twitter zikionyesha ndege kadhaa za jeshi la Anga la Marekani kwenye lami na akasema aliona ndege "zikitua na kupaa."
Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Florence Parly alisema ndege ya kwanza ya jeshi lake iliyokuwa imewabeba raia wa Ufaransa kutoka Afghanistan, ilitua usiku wa kuamkia Jumanne katika Falme za Kiarabu na kwamba serikali ya Ufaransa ilikuwa inajiandaa kutuma ndege zingine.
India ilihamisha wafanyakazi wa ubalozi wake nchini Afghanistan na raia wake wapatao 140 kwa ndege maalum ya kijeshi.
Jeshi la Marekani limethibitisha vifo vya watu wawili katika uwanja huo wa ndege. Jumatatu, rais wa Marekani Joe Biden alisema anasimama kidete na uamuzi wake wa kuondoa vikosi vya Marekani kutoka Afghanistan katika hotuba yake ya kwanza kwa umma tangu Taliban ilipouteka mji wa Kabul.
"Hatuwezi kwendelea kuwepo Afghanistan kwa kipindi kisicho na mwisho. Lengo letu kule lilikuwa kuhakikisha kwamba magaidi hawaishambulii Marekani," alisema kufuatia siku kadhaa za mjadala mkali baina ya Wamarekani kuhusu hali inayoendela nchini Afghanistan, huku baadhi wakikosoa jinsi ambavyo rais huyo amelishughulikia suala hilo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba "Ulimwengu unafuatilia matukio huko Afghanistan kwa karibu" na kwamba ana wasiwasi mkubwa kuhusu kile kitakachofuata."