Upande wa Serikali ulidai upelelezi bado haujakamilika. Hata hivyo Wakili wake Jebra Kambole Ijumaa ameitaka Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam kuhimiza waendesha mashtaka kukamilisha upelelezi katika wakati unaotakiwa.
Wakili Kambole pia amesema kuwa afya ya Kabendera inaendelea kudhoofika baada ya kupata tatizo la kupumua kila ifikapo usiku tangu Agosti 21, hali iliyopelekea kushindwa kutembea kwa siku mbili.
Gazeti la Mwananchi limeripoti kuwa wakili wake ameiomba Mahakama hiyo itoe amri kwa Jeshi la Magereza kumpeleka mtuhumiwa huyo Hospitali ya Taifa Muhimbili iliapatiwe matibabu.
Upande wa utetezi pia umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kulielekeza Jeshi la Magereza kumpeleka mteja wao kwenda kupimwa katika hospitali ya Serikali.
Kwa mujibu wa wakili wake usiku wa kuamkia Agosti 2, 2019 amesema : "Nilienda kumuona nikakuta amepooza mguu na kushindwa kutembea kwa siku mbili pamoja na kuishiwa nguvu, sisi kama mawakili na ndugu hatujui nini anachoumwa.”
"Kwa kuwa mteja wetu hajapata vipimo ambavyo vinastahili tunaomba Mahakama ielekeze Jeshi la Magereza mteja wetu akapimwe katika hospitali yoyote ya serikali ikiwemo Muhimbili penye vipimo vya uhakika," amedai Wakili Kambole.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.