Mkataba wa AfCTA uliosimamiwa na AU ulisainiwa nchini Rwanda na nchi 44 za Afrika mwaka 2018 ili kuimarisha biashara ndani ya bara hilo. Tangu wakati huo, nchi 54 za Afrika, ukiitoa Eritrea, zimesaini makubaliano hayo, na kuongeza wigo wa mkataba huo.
Achaleke Christian Leke, balozi wa vijana wa AU kwa ajili ya amani kwya Afrika ya Kati, ameiambia VOA kuwa AfCFTA itaisaidia Afrika kunufaika na rasilimali zake, bidhaa zenye ubunifu na soko la Afrika.
“Hata katika nchi ambapo wameendelea ( huko Afrika), nchi nyingine za Kiafrika haziwezi kunufaika nafikiri ndio maana fikra hii tukufu ya ukanda huru wa biashara Afrika ni muhimu sana na imekuja wakati muafaka,” Leke alisema.
Sekretarieti ya AfCFTA inakadiria kuwa muungano wa biashara huru wa kiwango cha dola za Marekani trilioni 3.4 unaweza kufikiwa miongoni mwa watu bilioni 1.3 Afrika.
AfCFTA inasema mkataba wa biashara una uwezo wa kuwanyanyua kimaisha watu milioni 30 kutoka katika lindi la umaskini huku ukipandisha viwango vya mapato kufikia dola za Marekani bilioni 450 ifikapo 2035.
Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) imezitaka nchi za Kiafrika kutekeleza mkataba wa eneo huru la biashara, likisema itatoa msukumo mkubwa kwa uzalishaji katika uchumi wa Afrika na kusaidia kutatua changamoto kama vile mabadiliko ya hali ya hewa.
Lakini wataalam kadhaa wanadai kuwa AfCFTA inaweza kuwa inaelekea kufeli iwapo viongozi wa Afrika hawatatua changamoto zilizopo katika bara hilo kama vile ufisadi uliokithiri na miundombinu mibovu. Leke anakubaliana nayo, lakini anatoa angalizo kuwa mkataba huo unahitaji kutekelezwa.