Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 12:51

Sudan: Wachambuzi Tanzania waitaka Umoja wa Afrika kuchukua hatua haraka


Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan
Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan

Wahadhiri wa diplomasia na wachambuzi wa siasa nchini Tanzania wameitaka  Umoja wa Afrika pamoja na umoja wa ushirikiano wa nchi za pembe ya Afrika IGAD  na jumuiya nyinginezo kuacha visingizio na kuendelea kukaa kimya kuhusu mgogoro wa Sudan.

Badala yake wamewataka wachukue hatua za haraka na kutoa azimio la pamoja dhidi ya mgogoro unaoendelea nchini humo huku pande zinazo zozana zikitakiwa kuangalia maslahi mapana ya taifa kwa kuwa madhara yake ni siyo kwa wananchi tu wa taifa hilo bali pia mataifa jirani.

Hatua ambayo mgogoro ulipofikia sasa ni dhahiri kuna hitajika hatua za haraka za mazungumzo baina ya pande mbili zinazo hasimiana ili kumaliza kile kinacho endelea na kuyanusuru maisha ya Wasudan ambao wanakimbia makazi yao huku vifo vikiripotiwa toka yaanze mapigano hayo.

Wanajeshi wa vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) huko Khartoum tarehe 23 Aprili 2023. Picha na Rapid Support Forces/ AFP.
Wanajeshi wa vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) huko Khartoum tarehe 23 Aprili 2023. Picha na Rapid Support Forces/ AFP.

Mhadhiri Deus Kibamba ambaye ni mbobezi wa masomo ya utatuzi wa migogoro kutoka chuo cha diplomasia Dar es Salaam amesema kwa kuwa pande zinazo zozana haziwezi kukaa chini na kumaliza tofauti zao, sasa ni wajibu wa mamlaka za jumuiya za Afrika kuwakalisha chini viongozi wa makundi hayo huku akiitaka AU kujitafakari kwa kushindwa hadi leo kuingilia kati mgogoro huo.

Kibamba anasema Umoja wa Afrika pale Addis Ababa unatunzwa kwa michango ya wanachama wa Umoja wa Afrika wakiwemo Watanzania tuna uhuru wa kuwauliza Addis Ababa mnafanya nini mpaka muache nchi inaungua ikiwa hamja ona bado haja yakuweza kuchukua hatua na kuweza kuingilia kati.

Wahadhiri wa diplomasia wanasema licha ya uhaba wa fedha unaoikabili Umoja wa Afrika na kusababisha changamoto kwa baadhi ya mataifa ambayo hayatoi michango yao kwa AU isiwe sababu ya wao kushindwa kuchukua hatua badala yake watafute mbinu yoyote ya haraka itakayoweza kuleta amani nchini humo.

Huku wachambuzi wa masuala ya siasa wakiendelea kuzitupia lawama asasi za kutetea haki za binadamu kwa kukaa kimya na wananchi wakipoteza maisha na kuwataka kuachana na tabia ya kuangalia pale palipo na maslahi yao kama anavyo sema mwanasheria Mbwana Aliamtu kutoka Arusha

Aliamtu: " Ikitokea mahali ambapo masilahi yakawa ni madogo au upande ukawa upo kwenye upande wao hawana utashi nao huwa wanapoteza pia nguvu ya kudai haki,watu wengi sasa wanakufa huko Sudan lakini hawazungumzi wala haichukuliwi hatua yeyote ya dharura."

Ama mgogoro wa Sudan unatazamwa kama sehemu ya muendelezo wa kugombania nafasi ya utawala ambayo bara la Afrika limekuwa muathirika wa matukio hayo kwa muda mrefu huku mataifa yenye nguvu yakihusishwa na mapigano yanayo endelea kuathiri jamii ya Wasudan.

Thabiti Mlangi mchambuzi wa siasa kutoka chuo cha sheria Tanzania akizungumza na Sauti ya Amerika amesema matatizo makubwa yanayo likumba bara la Afrika ikiwemo Sudan ni kwa baadhi ya viongozi kuwa na uroho wa madaraka.

Pia imani ya kuwa hakuna mtu mwingine atakaye weza kuongoza zaidi ya yeye suala ambalo Umoja wa Afrika inatakiwa kutumia kila njia ili kuhakikisha nchi hiyo ipo salama kwa kuwa wao ndio wamekuwa sababu ya mgogoro huo tangu walipo amua kuyaunganisha majeshi hayo mwaka 2021, alisema Mlangi.

Mlangi : "Watu wakisha onja zile raha za urais kutokuwa tayari kuuwachia na unaweza ukaona chanzo kikubwa cha huu mgogoro ni kwasababu tu kuna mmoja anaamini kwamba tokea mwaka 2019 baada ya hawa wanamgambo kuungana na jeshi la Sudan kumtoa Alibashiri lile baraza la usalama la Sudan sasa linastahili kuongozwa na Hemedt.

Hata hivyo Abbas Mwalimu mkufunzi kutoka Chuo cha Diplomasia Kurasini Dar es Salaam amesema kwa kuwa Umoja wa Afrika umeonyesha kushindwa sasa ni wakati wa Marais wastaafu kujitokeza na kuomba kusuluhisha mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo kwa kuwa kila nchi ina wazee ambao inawaamini.

Mkutano wa Umoja wa Afrika wakiwa katika kikao cha 35 cha kawaida huko Addis Ababa, Ethiopia, Jumomosi Feb 5, 2022.
Mkutano wa Umoja wa Afrika wakiwa katika kikao cha 35 cha kawaida huko Addis Ababa, Ethiopia, Jumomosi Feb 5, 2022.

Mwalimu: "Act Kuna haja kwao sasa kuona kwamba Afrika inahitaji kusuluhishwa yenyewe kupitia kwa wazee hao au watu ambao wameongoza nchi mbalimbali Afrika na hatimae kuweza kufikia hatima ya pamoja. Ni miaka ya karibuni Tabu Mbeki alikuwa akitumika lakini kuna haja ya wengine pia kuweza kutumika kuona kwamba migogoro ya Afrika inatatuliwa katika njia za amani."

Tangu kuanza kwa mapigano hayo Aprili 15 takribani watu 500 wameuawa na 5,000 kujeruhiwa kwa mujibu wa wizara ya afya ya Sudan suala ambalo Mbwana Aliamtu anaitaka Umoja wa Afrika kuamka pamoja na wanyonge kupaza sauti zitakazo weza kuleta mabadiliko ya kifikra na mfumo ili Afrika isonge mbele kutoka ilipo sasa.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Dar es Salaam.

XS
SM
MD
LG