Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 20:43

Tanzania: Viongozi waendelea kumkumbuka Bernard Membe


Hayati waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Tanzania Bernard Membe wakati wa uhaI wake kulia na nyuma yake ni rais wa zamani wa Tanzania Jakaya Kikwete.
Hayati waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Tanzania Bernard Membe wakati wa uhaI wake kulia na nyuma yake ni rais wa zamani wa Tanzania Jakaya Kikwete.

Wanasiasa viongozi wa dini na wasomi nchini Tanzania wameendelea kumkumbuka Membe kwa mchango wake katika siasa na uongozi huku wengi wao wakisema ni moja ya kiongozi wa kuigwa na aliyekuwa na msimamo juu ya kile ambacho anakiamini na hakuweza kukubali haki yake ichukuliwe na mtu mwingine. 

Miongoni mwao ni kiongozi wa Chama Cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe amesema kuna mambo mengi sana ya kuweza kujifunza kutoka kwake misimamo pamoja na utu wake.

‘‘Nadhani kuna vitu vingi sana vya kujifunza kutoka kwake hasa katika mgogoro wa Malawi alisimama bungeni na kusema Malawi mkituletea shida haitachukua siku mbili kuishika hiyo nchi kwa hiyo ana vitu vingi sana ambavyo ameshughulika navyo kwenye nchi yetu’’ amesema Zitto.

Ataendelea kukumbukwa kwa mengi aliyoyafanya wakati wa uhai wake hasa sifa yake ya kuweza kujenga matumaini kwa watu pale anapo kuwa anawaongoza kwa njia ya maneno jambo ambalo liliweza kumtofautisha na viongozi walio wengi wa Tanzania.

Akiyazungumzia maisha yake wakati wa uhai wake Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amesema alikuwa ana kipawa cha kuwajengea watu matumaini hata kama wana njaa au kiu.

‘‘Alikuwa na uwezo wa kujenga matumaini kwa watu kwa njia ya maneno na watu wakaweza kusubiria naweza kusema alikuwa na kipawa ambacho sio cha watu wote’’

Membe mpaka mauti yanamkuta bado alikuwa ni mwanachama wa chama cha mapinduzi,(CCM),na taarifa za kifo chake zilianza kusikika majira ya saa tano asubuhi siku ya Ijumaa kupitia vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii.

Huku taarifa za awali zilieleza kuwa Bernard Membe amefariki dunia baada ya kupata changamoto ya kifua na kupelekwa Hospitali ya Kairuki na baadaye kufariki dunia.

Kwa upande wa wachambuzi wa siasa wamesema wataendelea kujadili na kujifunza katika maisha aliyopitia wakati ni kiongozi na nje ya uongozi wake haswa kipindi alichotoka CCM na kwenda chama cha upinzani.

Nasoro Kitunda Mhadhiri kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam amesema ‘‘nadhani tunaweza tukajifunza hasa katika njia alizotumia kufikia mafanikio aliyoyapata lakini pia tusiache kujifunza katika makosa au changamoto zilizo mkabili katika njia zake alizopita hasa katika siasa’’.

Kiongozi huyo alizaliwa tarehe 9 Novemba mwaka 1953 akiwa ni mtoto wa pili katika watoto saba kwenye familia ya mzee Kamillius Anthony Ntachile na Mama Cecilia John Membe huko mkoani Lindi.

Membe ambaye anatajwa kuwa ni miongoni mwa wanasiasa makini na mwanadiplomasia nguli, aliwahi kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu 2020, kupitia chama cha upinzani ACT Wazalendo baada ya kukihama chama chake cha Mapinduzi (CCM).

ELIMU

Ilipofika mwaka 1962 Membe alianza elimu ya msingi katika shule ya Rondo-Chiponda na kuhitimu mwaka 1968, na kujiunga na masomo ya sekondari katika seminari ya Namupa (1969-1972), baadaye kuendelea Itaga Seminari iliyopo Tabora, kwa masomo ya kidato cha tano na sita (1973-1974). Huku shauku yake wakati wote huo wa masomo ni kuwa mtumishi wa kanisa (Padri).

Baada ya kumaliza masomo mwaka 1975 na 1977 Membe alijiunga na mafunzo ya jeshi la kujenga Taifa (JKT) kambi ya Oljoro, Arusha. Ilikuwa ni kwa mujibu wa sheria ambapo wanafunzi wote walio maliza elimu ya kidato cha sita walitakiwa kujiunga na jeshi kwa mwaka mmoja na ndipo Membe hakuweza tena kutimiza ndoto yake ya kuwa mtumishi wa Mungu na badala yake akaajiriwa katika Ofisi ya Rais, Utawala Bora.

Wakati yupo anaendelea na kazi mwaka 1978, Membe alipata Mafunzo ya sheria za Jinai na usalama wa nchi, nchini Uingereza na mwaka 1980, Membe alipata mafunzo ya siasa, katika Chuo cha Chama cha Mapinduzi (CCM), Kivukoni, Dar es Salaam.

Membe ametumikia nafasi mbalimbali katika siasa ikiwemo Kamanda wa Vijana CCM wa Mkoa wa Lindi, Mjumbe wa Kamati Kuu, na Katibu wa Secretarieti ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa chama hicho.

Na ilipofika mwaka 2000 alichaguliwa na wananchi wa Mtama kuwa mbunge kupitia jimbo la Mtama huku michango yake ndani ya bunge ikijielekeza katika masuala mbalimbali ya kuwasemea wananchi wake na taifa kwa ujumla.

Ilipofika mwaka 2005 akachaguliwa tena kuwa mbunge wa jimbo la Mtama na aliyekuwa Rais wa awamu ya nne Kikwete January 2006 alimteua kuwa naibu waziri wa mambo ya ndani.

Katika nafasi hiyo ya unaibu waziri wa mambo ya ndani Membe alikaa kwa muda wa miezi tisa na ilipofika mwezi wa kumi alihamishwa wizara na kuwa Naibu Waziri Nishati na Madini.

Ama ilipofika January 2007 Rais Kikwete alimteua Membe kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, baada ya aliyekuwa anashikilia wadhifa huo Dr Asha Rose Migiro, kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN).

Nafasi hiyo ya mambo ya nje Membe aliweza kudumu nayo kwa miaka nane mfululizo na kuwa Mtanzania wa pili kushika nafasi hiyo kwa muda mrefu akitanguliwa na Rais wa awamu ya nne Kikwete aliyedumu kwa miaka 10 mfululizo kama ambavyo kiongozi wa Chama Cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe alivyoeleza.

‘‘Baada ya Kikwete yeye ndio Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa aliyekaa kwa muda wa miaka 8 huku kikwete akitumikia miaka 10 katika wizara hiyo’’

Hata hivyo toka 2006, Membe alifanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali, zikiwemo Mwenyekiti Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Afrika, Mkuu wa Waangalizi wa Uchaguzi Mkuu Zimbabwe kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), na Mwenyekiti Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth).

Kugombea Urais na kuhama chama

Ilipofika tarehe 15, Julai mwaka 2020 Membe alijiunga na ACT Wazalendo huku akisukumwa na katiba ya chama hicho pamoja na itikadi yake kuwa ndivyo vilivyo mshawishi kuingia katika chama hicho na chama hicho kikampa nafasi ya kugombea Urais wa Tanzania na kupata jumla ya kura 81,129 ikiwa ni sawa na asilimia 0.5 ya kura zote.

Ilipofika mwezi wa kumi 2022 mwanadiplomasia huyo mbele ya Waziri Mkuu Kasim Majaliwa alieleza kuunga mkono utendaji wa Rasi Samia Suluhu Hassan na Machi 31,2022 chama cha mapinduzi CCM kilitangaza kumpokea na kumrejeshea uwanachama wake baada ya Kamati Kuu ya chama hicho chini ya uongozi wa Hayati John Magufuli, kuazimia kwa kauli moja na kumfukuza uwanachama.

Hadi mauti yanamfika Membe alikuwa ni Mwanachama wa chama cha mapinduzi CCM hata hivyo msemaji wa familia, Jaji Mustafa Ismail amesema maziko ya kiongozi huyo wa zamani katika wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe yanatarajiwa kufanyika Mei 16, 2023 kijijini kwao, Londo mkoani Lindi.

XS
SM
MD
LG