Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 07:05

Shambulio jipya la Marekani lilimlenga kiongozi wa Al-Shabab


Majengo ya shule katika eneo lililodaiwa kulipuliwa kwa bomu na Al-Shabaab huko Mogadishu, tarehe 25 Novemba 2021. Picha na AFP.
Majengo ya shule katika eneo lililodaiwa kulipuliwa kwa bomu na Al-Shabaab huko Mogadishu, tarehe 25 Novemba 2021. Picha na AFP.

Mkuu wa operesheni za nje katika kundi la Al-Shabab ndiye alikuwa mlengwa katika shambulizi jipya la anga lililofanywa na Marekani dhidi ya kundi hilo la wanamgambo, vyanzo viwili, akiwemo muasi wa kundi hilo la al-Shabab, waliiambia Sauti ya Amerika.

Afisa wa zamani wa al-Shabab, Omar Mohamed Abu Ayan aliiambia Sauti ya Amerika kuwa kamanda huyo mkongwe wa kijeshi Osman Mohamed Abdi, anayejulikana kama Moallim Osman, alikuwa mlengwa.

Jina la mlengwa na cheo chake pia vilithibitishwa na Wizara ya Habari ya Somalia katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne. Wizara hiyo ilisema Moallim Osman alikuwa akishughulikia upelekaji wapiganaji wa kigeni nchini Somalia ili kuisaidia al-Shabab.

Alionekana kunusurika katika shambulio la anga, msemaji wa Kamandi ya Marekani Afrika alisema.

"Kufuatia tathmini ya kina ya uharibifu wa vita, U.S.-AFRICOM imeonyesha kuwa kiongozi mmoja wa al-Shabab alijeruhiwa kutokana na operesheni hiyo," msemaji wa AFRICOM, Luteni Kamanda Timothy S. Pietrack, aliiambia Sauti ya Amerika siku ya Jumanne.

Shambulio hilo lilifanyika siku ya Jumamosi huko Jilib, ngome ya al-Shabab iliyoko takriban kilomita 385 kusini magharibi mwa Mogadishu.

"Tathmini ya awali ya kamandi ya kijeshi ni kwamba hakuna raia aliyejeruhiwa au kuuawa," taarifa ya AFRICOM ilisema.

Moallim Osman ni kamanda mkongwe ambaye ameshikilia nyadhifa kadhaa ndani ya kundi hilo la al-Shabab, ikiwa ni pamoja na kuwahi kuwa mkuu wa ulinzi, kulingana na afisa wa Somalia ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa kutokuwa na mamlaka ya kuzungumza na vyombo vya habari.

Maafisa wa Somalia pia wanasema Moallim Osman alihusika katika kupanga mashambulizi yaliyofanywa na kundi hilo Januari 2016 dhidi ya kambi ya kijeshi ya Umoja wa Afrika inayosimamiwa na vikosi vya Kenya huko El Adde.

Ni shambulio baya sana kufanywa na wanamgambo hao dhidi ya walinda amani nchini Somalia na lilifanyika katika mji alikozaliwa Moallim Osman, kulingana na vyanzo vya usalama vya Somalia.

Forum

XS
SM
MD
LG