Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 09:54

Mpaka kati ya Kenya na Somalia kufunguliwa


Waziri wa Mambo ya ndani wa Kenya Kithure Kindiki (kushoto) na Waziri wa Usalama wa Ndani wa Somalia, Mohamed Ahmed Sheikh Ali, wakiwa katika mkutano wa pamoja na waandishi wa jijini Nairobi, tarehe 15 Mei 2023. Picha na AFP.
Waziri wa Mambo ya ndani wa Kenya Kithure Kindiki (kushoto) na Waziri wa Usalama wa Ndani wa Somalia, Mohamed Ahmed Sheikh Ali, wakiwa katika mkutano wa pamoja na waandishi wa jijini Nairobi, tarehe 15 Mei 2023. Picha na AFP.

Kenya na Somalia Jumatatu zimekubaliana kufungua tena vituo vitatu vya mpaka kati ya nchi hizo mbili baada ya kufungwa kwa miaka 12 kutokana na ukosefu wa usalama na vitisho vinavyohusiana na ugaidi.

Ujumbe wa mawaziri watatu kutoka serikali ya shirikisho la Somalia uliowasili Kenya umekutana na waziri wa usalama wa Kenya Kithure Kindiki ambapo walikubaliana kufungua mpaka wa Mandera/Bulahawa jimbo la Mandera, mpaka wa Kiunga/Ras Kamboni, jimbo la Lamu na Liboi-Harhar/Dhobley jimbo la Garissa, ambayo ilifungwa na utawala wa Rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta mnamo 2011.

Hatua ya kufungwa kwa mpaka ilitokana na uvamizi wa mara kwa mara na mashambulizi yaliyopangwa na kundi la kigaidi la al Shabaab, na kusababisha Kenya kutuma jeshi lake Somalia kuzuia mashambulizi zaidi.

Katika mkutano huo wa ngazi ya juu wa mawaziri, Kindiki alikutana na Waziri wa Usalama wa Ndani, Serikali ya Shirikisho la Somalia Mohamed Ahmed Sheikh Ali, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Abdulkadir Mohamed Nur na Abshir Omar Jama, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, katika ofisi ya rais jijini Nairobi.

Mkutano huo pia luhudhuriwn na Waziri wa Ulinzi wa Kenya Aden Duale na maafisa wengine wakuu wa serikali.

Waziri Kindiki ametangaza kuwa Kenya na Somalia zimeazimia ndani ya siku thelathini kufungua mpaka wa Mandera-Bulahawa. Na katika kipindi cha ndani ya cha siku 60 watafungua mpaka wa Liboi-Harhar/Dhobley na katika kipindi cha siku 90 kufungua mpaka wa Kiunga-Ras Kamboni. Vituo vyote viliyofungwa miaka kumi na mbili iliyopita.

Pamoja na kuwa mipaka hiyo ilifungwa rasmi wakati huo, wahalifu na wahamiaji bado wamekuwa wakitumia hususani wanamgambo wa al-Shabaab walio na makao yao nchini Somalia.

Katika mkutano huo wa mawaziri wa nchi hizo mbili umelenga kufungua mipaka hiyo kwa lengo la kuimarisha usafiri wa watu na bidhaa pamoja na kudumisha na kukuza ushirikiano wa kikanda, na maendeleo endelevu kati ya nchi hizo.

Mkutano huo pia ulilenga kudhibiti uhamiaji usio wa kawaida, uhalifu na itikadi kali za kigaidi na pia kurahisisha mahitaji ya visa, na ufanyaji wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili jirani kama anavyoeleza Mohamed Ahmed Sheikh Ali, waziri wa Usalama wa Ndani, Serikali ya Shirikisho la Somalia.

Aidha, mawaziri hao wamekubaliana kuimarisha mawasiliano ya mipakani na kubadilishana habari, kubuni mbinu za kutatua changamoto za mipakani kwa kufahamu asili ya vitisho vya kimataifa ambavyo vinahitaji uratibu na majibu ya kina ili kujenga imani kwa umma na ushirikiano kuhakikisha mafanikio katika juhudi za ushirikiano wa kuvuka mpaka.

Rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud tarehe 15 Julai mwaka jana, walikubaliana kuendelea kuweka utaratibu wa kufungua mipaka na kubuni juhudi za pamoja kukabili tishio la ugaidi la wanamgambo wa al shabaab. Hii inatajwa kuwa ni muendelezo wa mashauriano hayo.

KENNEDY WANDERA, SAUTI YA AMERIKA, NAIROBI.

XS
SM
MD
LG