Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 14:52

Nchi za Afrika zenye ushawishi zatakiwa kuhusika kukomesha mapigano Sudan


Moshi ukifuka katika jiji la Khartoum wakati mapigano yakiendelea tarehe 11, Mei 2023. Picha na shirika la habari la AFP.
Moshi ukifuka katika jiji la Khartoum wakati mapigano yakiendelea tarehe 11, Mei 2023. Picha na shirika la habari la AFP.

Mkuu wa shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa Volker Turk amezisihi nchi zenye ushawishi barani Afrika kuzishawishi pande zinazozozana nchini Sudan kukomesha mapigano yaliyoanza mwezi uliopita.

Akihutubia kikao cha dharura cha Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Turk alisema mzozo umesababisha "mateso haya makubwa kuwa janga."

"Ninalaani matumizi ya ghasia yanayofanywa na watu ambao hawathamini maisha na haki za msingi za mamilioni ya raia wenzao," Turk alisema.

Mapigano katika mji mkuu wa Sudan yalizidi kuwa mbaya siku ya Jumatano, wakati mashahidi wakiripoti kuwepo kwa mashambulizi ya anga, roketi na milio ya risasi katika vitongoji kadhaa.

Jeshi la Sudan, likiongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, lilishambulia maeneo ya Khartoum na ya miji dada miwili, Omdurman na Bahri.

Jeshi la Sudan linajaribu kuwatimua wanajeshi wa Rapid Support Forces, wanaoongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, ambao wamejificha katika maeneo ya makazi ya watu ambayo wamekuwa wakiyashikilia tangu mapigano yalipoanza katikati ya mwezi Aprili.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani, mzozo huo umesababisha vifo vya watu zaidi ya 600 na wengine zaidi ya 5,000 kujeruhiwa.

Wajumbe kutoka jeshi na kikosi cha RSF wamekuwa wakikutana nchini Saudi Arabia kwa takriban wiki moja. Mwanadiplomasia wa Magharibi anayeyafahamu mazungumzo hayo aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa wapatanishi walikuwa wakilenga makubaliano ya kusitisha mapigano ili misaada ya kibinadamu iweze kufikiwa.

Waziri mdogo wa mambo ya nje wa Marekani Victoria Nuland amesema wapatanishi wa Marekani walikuwa na "matumaini lakini wanaangalia kwa tahadhari" katika masuala yote mawili.

Baadhi ya habari katika taarifa hii zinatoka katika mashirika ya habari ya Associated Press, Reuters and Agence France-Presse.

XS
SM
MD
LG