Ulaya, Asia zafarijika kwa kupanda bei za hisa kutokana na COVID-19 kudhibitiwa

Wafanyabiashara wa sarafu wakifuatilia bei za fedha za kigeni katika benki ya KEB Hana, Seoul, Korea Kusini, Jumatatu, Aprili 27, 2020. Masoko ya hisa ya Asia yalipanda baada ya benki kuu ya Japan kuahidi kununua bondi.

Bei za hisa katika masoko ya Ulaya na Asia zimepanda Jumatatu kufuatia habari za kuanza kupunguzwa kwa masharti ya watu kutotoka nje kutokana na kupungua kwa maambukizi ya COVID-19.

Kwa upande mwengine kupanda kwa Lisa kunatokana na huko Ulaya kuwepo matumaini kwamba mashirika ya ndege yatapata msaada mkubwa wa fedha kunusuru usafiri wa ndege.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Uingereza Reuters hisa za shirika la ndege la Ujerumani Luftansa zilipanda kwa asilimia 6.5 baada ya Waziri wa uchukuzi wa nchi hiyo kusema serikali iko tayari kulisaidia shirika hilo.

Kwa upande wa benki za Ulaya hisa zilipanda kwa asilimia 4.1 baada ya benki ya Deutche Ujerumani kutangaza faida kubwa ambayo haikutarajiwa kwa robo ya kwanza ya mwaka 2020.

Na huko Asia hisa zilipanda baada ya benki ya Japan kutangaza msaada zaidi wa kufufua uchumi kutokana na janga la corona.

Wakati huohuo serikali ya Iraq imetangaza inatafakari juu ya kupunguza mishahara ya wafanyakazi katika bajeti inayotayarishwa upya kutokana na kupunguka sana kwa bei za mafuta.

Katika muswada wa awali wa bajeti yake serikali ilikuwa inategemea sana mapato ya mafuta wakati pipa moja lilikuwa linauzwa kwa dola 56 ili kugharimia miradi yake muhimu.

Lakini hii leo bei kwa pipa iko kati ya dola 20 hadi 30. Moja wapo ya mapendekezo ya serikali ni kupunguza kwa hadi aslimia 50 ya mishahara ya maafisa wa juu ambapo itaweza kunusuru mamilioni ya dola kulingana na afisa wa serikali aliyezungumza bila ya kutaka kutajwa.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.