Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:09

Corona Afrika: Maambukizi Tanzania yavuka 250, Zimbabwe yaongeza muda wa kukaa nyumbani


Mhudumu wa afya nchini Nigeria apima joto la mwanamke ili kubaini iwapo huenda anaugua.
Mhudumu wa afya nchini Nigeria apima joto la mwanamke ili kubaini iwapo huenda anaugua.

Tanzania ilitangaza Jumatatu kwamba watu 87 zaidi wameambukizwa virusi vya Corona na kufikisha jumla ya wagonjwa 257 nchini humo. Idadi ya wagonjwa imeongezeka kutoka 147 iliyotangazwa awali, hadi 257.

Taarifa ya wizara ya afya inasema kwamba kati ya walioambukizwa,16 wapo visiwani Zanzibar.

“Wagonjwa wote walioripotiwa Tanzania bara wanaendelea vizuri isipokuwa wagonjwa wanne wanaopatiwa huduma za wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum”, imesema taarifa ya wizara ya afya ya Tanzania, iliyosainiwa na waziri wa afya Ummy Mwalimu.

Idadi kubwa ya maambukizi yameripotiwa jijini Dar-es-salaam, ikifuatiwa na Arusha, Dodoma, Mbeya, Kilimajaro, Pwani, Tanga na Manyara.

“Tunasikitika kutangaza vifo vitatu vilivyotokea jijini Dar es salaam vya watu waliothibitishwa kuwa na maambukizi ya COVID-19,” imemalizia kueleza taarifa ya wizara ya afya ya Tanzania.

Nchini Kenya wamekataa mpango wa kufungua shughuli katika mahakama ambazo hazina teknolojia ya mawasiliano kupitia kwa njia ya video.

Gazeti la Business daily linaripoti kwamba Jaji mkuu David Maraga, alitangaza kwamba vikao vya mahakama vitafanyika katika sehemu za wazi kuanzia jumatano, punde tu baada ya wizara ya afya kuidhinisha pendekezo hilo.

Lakini miungano ya wafanyakazi katika idara ya mahakama, wamesema afya ya wanachama wao ni muhimu zaidi, wakitaka mwelekeo maalum kuwekwa kabla ya shughuli za mahakama kufunguliwa tena.

Wanataka sehemu zote mahakamani kunyunyuziwa dawa, idadi ya watu wanaohudhuria vikao kudhibitiwa, na wafanyakazi ambao hawana magari binafsi, kusafiriswa na magari ya idara hiyo kutoka nyumbani hadi kazini na kurejea, wafanyakazi wenye umri wa zaidi ya miaka 58 kuruhusiwa kufanya kazi wakiwa nyumbani, miongoni mwa masharti mengine.

Nchini Ghana rais Nana Akufo Addo, amelegeza masharti ya kuzuia watu kusafiri kutoka sehemu moja ya nchi hadi nyingine, akiendelea kuwahimiza watu kuvaa barakoa.

Marufuku ya watu kukusanyika na shule kufunguwa, itaendelea kutumika.

Mipaka ya Ghana itaendela kufungwa kwa wiki mbili zaidi ili kudhibithi maambukizi ya virusi vya Corona.

Rais Akufo Addo, amesema uamuzi wake umetokana na hali ya kuelewa jinsi virusi vya Corona vinavyosambaa , akisema mafanikio yatatokana na kuongeza idadi ya vipimo, na wagonjwa kupewa matibabu.

Nchini Zimbabwe, Rais Emmerson Mnangagwa ametangaza kuongeza mda wa watu kusalia makwao kwa wiki mbili zaidi.

Hata hivyo, shughuli katika machimbo ya madini na utengenezaji wa bidhaa zitaendelea lakini kwa kiwango kidogo.

Amri ya kwanza ya watu kusalia nyumbani, ilikamalika Jumapili.

Katika hotuba ya moja kwa moja kupitia televisheni, Mnangagwa amesema lengo kubwa la kuweka amri hiyo, halijafanikiwa, kabla ya kuongeza kwa siku 14 zaidi.

Ametaja hatua ya kuongeza mda huo kuwa uamuzi mgumu, lakini muhimu sana katika kuzuia maambukizi na vifo kutokana na virusi vya Corona.

Rais wa Mali Boubou Cisse, ametetea uamuzi wa kuandaa awamu ya mwisho ya uchaguzi wa bunge, akisema ni fursa nzuri ya kurejesha nchi hiyo katika hali ya utulivu.

Awamu ya kwanza ya uchaguzi huo, uliocheleweshwa sana, ilifanyika wiki tatu zilizopita licha ya mashambulizi na vitisho kutoka kwa makundi ya wanamgambo.

Wanasiasa wa upinzani wamekumbana na vitisho, ikiwemo kutekwa nyara kwa kiongozi wa upinzani Soumalia Cisse.

Mali, nchi yenye huduma mbaya za afya, iliandaa uchaguzi jumapili, licha ya janga la virusi vya Corona.

Nchini Nigeria visa vipya 86 vya maambukizi ya virusi vya Corona vimeripotiwa.

Maafisa pia wameripoti vifo vya watu 21.

Nigeria imetangaza kuongeza kasi ya kufanya vipimo vya Corona kati ya raia wake na kuonya kwamba huenda idadi ya maambukizi ikaongezeka sana.

Watu 627 wameambukizwa virusi vya Corona na 21 kuaga dunia nchini Nigeria, yenye idadi ya juu zaidi ya watu Afrika.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG