Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 20:42

Mkusanyiko wa habari za Covid -19 Barani Afrika


Mhudumu wa afya amfanyia vipimo mwanamke huyu ili kubaini kama ana dalili za ugonjwa wa Corona.
Mhudumu wa afya amfanyia vipimo mwanamke huyu ili kubaini kama ana dalili za ugonjwa wa Corona.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alisema Jumatano kwamba watu waliorekodiwa kwa video wakihepa kutoka karantini jijini Nairobi watakamatwa na kurejeshwa kwa karantini ili wamalize mda wao waliotakiwa kujitenga.

Kenyatta alisema hayo baada ya video inayoonyesha watu wanaoruka ukuta kutoka katika kituo cha karantini kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Vyombo vya Habari vya Kenya vliripoti kwamba watu 50 walihepa kutoka Karantini japo serikali haijathibitisha idadi hiyo.

Kenyatta alisema serikali inawafahamu wote waliohepa.

Tanzania

Nchini Tanzania idadi ya watu ambao wamethibitisHwa kuambukizwa virusi vya Corona iliongezeka Jumatano na kufikia 284. Kulingana na takwimu za serikali, watu 10 walikuwa wamekufa kufikia wakati tunaandaa ripoti hii.

Maombi maalum yalifanyika kuombea taifa hilo dhidi ya janga la Corona.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alihudhuria ibada hiyo alihimiza umuhimu wa wananchi kuendelea na shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo ili kupunguza athari za uchumi zinazosababishwa na janga la Corona.

Maambukizi ya Corona yameripotiwa katika mikoa 17 ya Tanzania.

Watu wote anatakiwa kuvaa barakoa, wakiwa katika shughuli za kawaida ili kudhibithi maambukizi.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo - DRC

Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo inatarajiwa kulegeza masharti yaliyowekwa kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona, hasa katika mji mkuu wa Kinshasa ambao umerekodi visa vingi vya maambukizi ya virusi vya Corona nchini humo.

Benki na maduka yanayouza vyakula, yanatarajiwa kufunguliwa tena katika sehemu ya Gombe, kitovu cha maambukizi ya Corona DRC.

Shughuli katika sehemu hiyo zimekuwa zimefungwa kwa mda wa wiki mbili.

Wagonjwa 30 wa Corona walithibithishwa wakati shughuli za kawaida zilikuwa zimesitishwa Gombe, na asilimia 80 ya watu waliokaribiana na wale walioambukizwa kupatikana.

Polisi wameeka vizuizi barabarani, kuzuia watu kuingia na kutoka Gombe.

Wafanyakazi maalum wenye vibali, ndio wanaruhusiwa kuingia na kutoka sehemu hiyo.

Nchini Rwanda, mkutano wa jumuiya ya Madola, uliokuwa umepangwa kufanyika mjini Kigali, Rwanda, umeahirishwa kutokana na janga la Corona. Zaidi ya wajumbe 10,000 wakiwemo viongozi wa nchi mbalimbali, walitarajiwa kuhudhuria mkutano huo wa 26 wa jumuiya ya madola, katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Mkutano huo ulikuwa umepangiwa kufanyika kuanzia tarehee 22 hadi 27 June mwaka huu.

Tarehe mpya haijatangazwa.

Hii ingekuwa mara ya kwanza kwa mkutano huo kufanyika katika nchi ambayo haikuwa koloni la Uingereza.

Uganda

Uganda imeongeza idadi ya watu ambao wameambukizwa virusi vya Corona, kutoka 56 hadi 61, kulingana na takwimu za Jumatano.

Hii ni baada ya kuongeza dereva wanne wa magari ya kubeba mizigo kutoka Kenya, na mmoja kutoka Tanzania, waliogunduliwa kuambukizwa baada ya kuingia nchini humo.

Uganda ilianza kuwapima madereva wa magari ya kubeba mizigo, wiki mbili zilizopita.

Madereva hao wanapimwa na kuruhusiwa kuendela na safari zao, huku wakifuatiliwa.

Iwapo vipimo vinabaini kwamba wameambukizwa Corona, wanawekwa karantini.

Awali, Uganda haikuwa inajumulisha madereva kutoka nje, wanaopatikana kuambukizwa Corona, kwa idadi ya wagonjwa nchini humo na badala yake imekuwa ikiwarudisha katika nchi wametoka.

Wizara ya afya a Uganda imesema kwamba shirika la afya duniani limetoa mwelekeo kwamba kila kisa cha maambukizi kinahesabiwa katika nchi kimeripotiwa.

Kulingana na wizara ya afya ya Uganda, kati ya madereva wa magari ya kubeba mizigo 70 na 1,000 hufanyiwa vipimo nchini Uganda kila siku.

Afrika Kusini

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, alitangaza kutenga kiasi cha dola bilioni 26 kusaidia kampuni na wafanyakazi milioni 3 wakati huu wa janga la Corona.

Katika hotuba kwa taifa kupitia televisheni siku ya Jumatano, Ramaphosa alisema msaada huo wa kifedha ni kiasi cha asilimia 10 ya mapato ya jumla ya Afrika kusini.

Pesa hizo zitatolewa kwa bajeti ya taifa, lakini amesema pia kwamba serikali yake inafanya mazungumzo na benki kuu ya dunia Pamoja na shirika la fedha duniani IMF, kwa msaada zaidi.

Ramaphosa amsema kwamba msaada wa kifedha unahusu msamaha wa kulipa ushuru, kulipa mishahara kupitia kwa bima ya kukosa ajira na kufadhili biasahra ndogondogo.

Lesotho

Waziri mkuu wa Lesotho Thomas Thabane, ameongeza mda wa watu kusalia nyumbani kwa wiki mbili zaidi ili kudhibithi maambukizi ya virusi vya Corona.

Nchi hiyo, haijaripoti kisa chochote cha maambukizi ya Corona, lakini amri ya watu kusalia makwao imekuwa ikitekelezwa kwa mda wa wiki tatu zilizopita.

Amri hiyo itaendelea kutekelzwa hadi May tarehe 5.

Waziri mkuu Thabane amesema kwamba hatua ya kuongeza mda wa kusitisha shughuli za kawaida, itatoa fursa kwa serikali kujipanga vyema jinsi ya kushughulikia janga hilo endapo litatokea nchini humo.

Zimbabwe

Nchini Zimbabwe wafanyabiashara katika maduka ya reja reja, wamekubaliana kupunguza kabisa bei ya bidhaa muhimu ili kuwasaidia watu, nchi hiyo inapopitia wakati mgumu zaidi wa kiuchumi kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Wizara ya Habari imesema kwamba Habari zaidi kuhusu mpango huo zitatolewa baadaye.

Mfumuko wa bei umeongezeka nchini Zimbabwe na kufikia asilimia 676 mwezi Machi, kutoka asilimia 540 mwezi Februari.

Zimbabwe, ambayo inaagiza kiasi kikubwa cha chakula kutoka nje ya nchi, inakabiliwa vile vile na uhaba wa sarafu za nje.

Bei ya vyakula imeendelea kuongezeka katika wiki za hivi karibuni.

Bei ya mkate imeongezeka kutoka dola 20 za Zimbabwe had idola 30.

Nigeria

Magavana katika majimbo ya kaskazini mwa Nigeria, wamekubaliana kufunga shule za kiislamu zinazotoa mafunzo kwa mamilioni ya vijana katika eneo hilo, kutokana na janga la virusi vya Corona.

Katika taarifa ya Pamoja, magavana hao wamesema kwamba hatua ya kufunga shule hizo inatokana na hatari kubwa iliyopo ya maambukizi, na kwamba Watoto waliokuwa katika shule hizo watarudishwa kwa wazazi wao.

Watoto mayatima watasaidiwa na serikali za majimbo katika sehemu watakapopelekwa.

Kulingana na takwimu rasmi, chini ya nusu ya Watoto kaskazini mwa Nigeria, huhudhuria masomo katika shule za serikali.

Familia nyingi nchini Nigeria ni maskini, zikiishi kwa chini ya dola mbili kwa siku, sababu inayopelekea familia hizo kutegemea shule za kiislamu kwa msaada wa masomo na mahitaji mengine ya kibinadamu.

Kulingana na shirika la haki za kibinadamu nchini Nigeria, karibu wanafunzi milioni 100 wanategemea shule za kiislamu kwa masomo na msaada muhimu wa kibinadamu kama chakula.

Ghana na Burkina Faso

Ghana na Burkinafaso zimeanza kulegeza masharti ya watu kukaa nyumbani na kusitisha shughuli za kawaida, kama hatua ya kufanyia majaribio uwezekano wa kurejea shughuli za kawaida kutokana na janga la Corona.

Hatua hiyo inachukuliwa na nchi hizo baada ya siki kadhaa za kusitisha shughuli za kawaida na kuathiri uchumi.

Nchi hizo za Afrika magharibi zimekuwa zikirekodi ongezeko la watu wanaoambukizwwa virusi vya Corona, na haijulikani namna zitakavyokabiliana na maambukizi hayo.

Idadi ndogo sana ya watu wamepimwa Afrika kujua iwapo wameambukizwa virusi vya Corona.

Kuna hofu kwamba huenda virusi vya Corona vikasababisha maafa makubwa Afrika katika siku za hivi karibuni.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC.

XS
SM
MD
LG