Polisi walimkamata mwandishi Kabendera jijini Dar es Salaam kwa shutuma za uhalifu wa kupanga, kushindwa kulipa kodi na utakatishaji fedha. Mawakili wake wamekana mashtaka yote.
Kesi yake bado haijaanza. Kila anapofikishwa mahakamani tangu mwezi Agosti, upande wa waendesha mashtaka wamekuwa wakiiambia mahakama kwamba uchunguzi wao haujakamilika.
Mwezi uliopita, wakili wa Kabendera, Jebra Kambole ameiambia mahakama kwamba alikuwa akijaribu kufikia muafaka na upande wa mashtaka. Jumatano, Kambole aliiambia mahakama kwamba utaratibu huo bado haujafikia mwisho.
Makundi ya kutetea haki yanasema uhuru wa habari umeminywa sana tangu Rais John Magufuli alipochukuwa madaraka mwaka 2015. Chini ya utawala wake serikali imefunga magazeti kadhaa na tovuti pamoja na kuwakamata viongozi wa upinzani na kuweka masharti kwa mikutano ya kisiasa.
Serikali inapinga vikali ukosoaji kwamba inakandamiza vyombo vya habari.