Polisi Haiti watoa maelezo juu ya genge lililowateka Wamishonari

Ramani ya Haiti

Genge baya sana linalojulikana kwa kuteka watu nyara na mauaji nchini Haiti, limeshutumiwa na polisi kwa kuwateka nyara wamishionari 17 kutoka shirika la Kimarekani.

Watoto watano wanaaminika kuwa miongoni mwa watu waliotekwa nyara.

Mkuu wa polisi wa Haiti Frantz Champagne amesema kwamba kundi la kihalifu kwa jina Mawozo 400 linaripotiwa kuwateka nyara kundi hilo la wamishonari katika sehemu ya Ganthier, mashariki mwa mji mkuu wa Port-au-Prince.

Genge hilo limelaumiwa kwa kuwateka nyara makuhi watano na watawa wawili, mapema mwaka huu, nchini Haiti.

Genge hilo linadhibithi sehemu za Croix-des-bouguests, ambayo pia inahusisha Ganthier, ambapo hutekeleza utekaji nyara wa watu na magari, pamoja na kuwatoza pesa wafanyabiashara.

Kanisa la Wainjilisti la Ohio hapa Marekani, limesema kwamba waliotekwa nyara ni raia 16 wa Marekani na raia mmoja wa Canada, watoto watano, wanawake watano na wanaume watano.

Waliotekwa nyara walikuwa safarini kutembelea watoto mayatima.

Ofisi ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kwamba ina habari kuhusu utekaji nyara huo, na kwamba maslahi na usalama wa raia wa Marekani walio nje ya nchi ni mojawapo ya mambo muhimu ya wizara ya mambo ya nje.