Nchi za Magharibi zalaani kukamatwa wanasiasa Sudan

FILE - Waandamanaji wakipiga mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Oktoba, Khartoum, Sudan, Jan. 9, 2022.

Nchi za Magharibi zimeshutumu kukamatwa hivi karibuni kwa wanasiasa wa ngazi ya juu nchini Sudan wakati maandamano ya kupinga jeshi yakiendelea Alhamisi.

Uingereza, Marekani , Umoja wa Ulaya na wengine wamesema kutiwa ndani kwa viongozi hao ilikuwa ni ishara ya kushtua na imetoa wito wa kuachiliwa haraka kwa wale wote waliokamatwa.

Maafisa wa polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wanaandamana Alhamisi kupinga mapinduzi ya Octoba mwaka 2021 na kukamatwa kwa hivi karibuni kwa waandamanaji na wanachama wa makundi ya kiraia.

Khalid Omer Yousif na Wagdi Salih ambao wamekuwa wakosoaji wakubwa kwa jeshi, walikamatwa na vikosi vya usalama Jumatano.

Wanaharakati wanaopinga mapinduzi wamesema zaidi ya watu 2,000 wakiwemo waandishi wa habari wanachama wa jumuiya za kiraia na wafanyakazi wa kibinadamu wamekamatwa na wengine wameshikiliwa bila kushitakiwa tangu jeshi lilipopindua serikali ya kiraia takriban miezi minne iliyopita.

Mazungumzo yanayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kumaliza mizozo ya kisiasa yamekwama, huku makundi kadhaa yakikataa kuwa sehemu ya mashauriano hayo.