Mjumbe maalum wa Marekani kwa Pembe ya Afrika atafanya ziara Saudi Arabia, Sudan na Ethiopia wiki ijayo huku migogoro ikiwa inaendelea katika mataifa mawili ya Afrika, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza Ijumaa.
David Satterfield na naibu waziri wa mambo ya nje Molly Phee watasafiri kwenda Riyadh, Khartoum na Addis Ababa kuanzia Januari 17 hadi 20.
Huko Riyadh, wawili hao watakutana na kundi la Marafiki wa Sudan, linalotoa wito wa kurejeshwa kwa serikali ya mpito ya nchi hiyo kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Oktoba.
Mkutano huo unalenga uungaji mkono wa kimataifa kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa kufanikisha kufufua tena kipindi cha mpito cha kiraia kuelekea demokrasia nchini Sudan, kulingana na taarifa hiyo.