Maelfu ya waandamanaji wanaounga mkono jeshi la Sudan waliandamana Jumatano kupinga azma ya Umoja wa Mataifa ya kutatua mzozo wa kisiasa nchini humo, miezi mitatu baada ya mapinduzi, mwandishi wa shirika la habari la AFP aliripoti.
Waandamanaji hao walikusanyika nje ya ofisi ya Tume ya Umoja wa Mataifa wa Usaidizi wa Mpito kwa Sudan (UNITAMS) ambayo ilikuwa imeanzisha mazungumzo na makundi ya Sudan mwezi huu.
Walibeba mabango yaliyosomeka “Down, down UN” na mengine yakimtaka mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa, Volker Perthes aondoke kurudi nchini kwake. Hatutaki uingiliaji wan je katika nchi yetu, mmoja wa waandamanaji Hamed al-Bashir aliiambia AFP nje ya ofisi za Umoja wa Mataifa.
Januari 10, Perthes alisema mashauriano yanalenga kuwaunga mkono wasudan kufikia makubaliano juu ya njia ya kutoka kwenye mzozo wa sasa. Lakini pia alibainisha kuwa Umoja wa Mataifa haujawasilisha pendekezo lolote, rasimu, au dira ya suluhisho.