Takriban watu 78 wamekufa na mamia kujeruhiwa wakati wa operesheni ya kuzuia waandamanaji wanaopinga mapinduzi, wakati mamlaka zimewakamata mamia ya wanaharakati wanaodai demokrasia, hiyo ni kwa mujibu wa kundi huru la madaktari nchini humo.
Wanaharakati wapenda demokrasia wameongeza wito wao wa kutaka kurejeshwa utawala wa kiraia tangu jeshi lilipochukua madaraka Oktoba 25 mwaka jana likiongozwa na jenerali Abdel Fattah al-Burhan.
Mapinduzi hayo yamechelewesha utayarishaji wa ushirikiano wa madaraka, baina ya jeshi na raia ambayo yamekuwa yakijadiliwa tangu mwaka 2019 baada ya kupinduliwa kiongozi wa muda mrefu Omar al Bashir.
Maandamano ya Jumapili yalifanyika katika mji mkuu wa Khartoum, maeneo jirani ya Omdurman, katika jimbo la Gedaref upande wa mashariki, na miji ya kaskazini ya Atbara na Dangola hiyo ni kwa mujibu wa mashahidi.
Maafisa wa usalama wa Sudan wameonya waandamanaji waliokuwa wanaelekea katikati ya mji mkuu wa Khartoum wakati vikosi vya usalama vikifunga mitaa inayoelekea katika makazi ya rais.
lakini waandamanaji katika mji mkuu walikuwa kwa kundi kubwa wakati wakielekea katika makazi hayo na polisi walifyatua mfululizo wa gesi ya machozi wakati wakiwasili katika eneo hilo.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP