Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 04:51

UN yafuatilia kwa karibu ghasia zinazoendelea nchini Sudan


Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameshutumu ghasia zinazoendelea kuongezeka nchini Sudan.

Msemaji wa Guterres, Stephanie Dujaric, amewaambia waandishi wa habari mjini New York kwamba UN inafuatilia kwa karibu sana hali ilivyo nchini Sudan.

Dujarric ameeleza kuwa: "Naweza kusema kwamba tunafuatilia kwa karibu sana hali ilivyo nchini Sudan. Katibu mkuu Guteres amelaani ghasia zinazoendelea nchini humo hasa zinazowalenga waandamanaji, na amewataka majeshi ya usalama kutotumia nguvu na kuheshimu haki na uhuru wa raia wa kuandamana na kujieleza.

Katibu mkuu pia ametilia mkazo hatua ya kujiuzulu kwa Waziri mkuu Abdalla Hamdok na kuelezea masikitiko kwamba hakujapatikana maelewano ya kisiasa licha ya hali kuendelea kuwa mbaya nchini sudan. Katibu mkuu anawashawishi washirika wote kuendelea kujadiliana ipasavyo ili kufikia makubaliano yanayowahusu wote, kwa ajili ya amani ya kudumu."

Raia wa Sudan wamejitokeza barabarani katika mji mkuu wa Khartoum na miji mingine katika maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi huku nchi hiyo ikiingia katika mgogoro zaidi wa madaraka, kufuatia kujiuzulu kwa Waziri mkuu Abdalla Hamdok.

Maafisa wa usalama wametumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji katika mijikadhaa ikiwemo katika sehemu zilizo karibu na ikulu ya rais.

Mapambano kati ya maafisa wa usalama na waandamanaji yamekuwa yakishuhudiwa karibu na ikulu ya rais tangu Oktoba 25, mapinduzi yalipotokea.

Waandamanaji wamekuwa wakirusha mawe huku maafisa wa usalama wakitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya.

Hakuna ripoti za vifo wala majeruhi zimetolewa kufikia sasa.

Waziri Mkuu Abdalla Hamdok alijiuzulu jumapili akisema kwamba ameshindwa kufikia makubaliano kati ya magenerali katika jeshi na watetezi wa demokrasia.

XS
SM
MD
LG