Polisi wa Sudan Ijumaa wamesema maafisa wa usalama waliwaua kwa risasi watu wanne siku ya Alhamisi wakati wakuzima maandamano ya nchi nzima dhidi ya utawala wa kijeshi.
Maafisa wa usalama walitumia gesi ya kutoa machozi na maguruneti kwa waandamanaji mjini Khartoum na katika miji jirani ya Omdurman na Bahri kuelekea ikulu ya rais siku ya Alhamisi, walioshuhudia na shirika la habari la Reuters walisema.
Polisi wamesema katika taarifa kwamba watu wanne waliuawa huko Omdurman na waandamanaji 297 na maafisa wa polisi 49 walijeruhiwa katika maandamano ya nchi nzima, ambayo yalijumuisha maelfu ya watu.
Televisheni ya Al Hadath ilimnukuu mshauri wa kiongozi wa kijeshi Abdel Fattah Al-Burhan akisema jeshi halitamruhusu mtu yeyote kuitumbukiza nchi katika machafuko na kwamba maandamano yanayoendelea, ni “tatizo kubwa la kimwili, kisaikolojia na kiakili kwa nchi” na hayatosaidia kufikia suluhu ya kisiasa.
Maandamano ya Alhamisi yalikuwa maandamano makubwa kwa mara ya 11 tangu mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 25 ambayo yalipelekea waziri mkuu Abdala Hamdok kuondolewa kwenye wadhifa wake na baadaye akarejeshwa.
Waandamanaji walilitaka jeshi lisiwe na jukumu lolote katika serikali wakati wa uongozi wa mpito kuelekea uchaguzi huru.