Huduma za internet zilionekana kuleta hitilafu katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum leo Alhamis kabla ya maandamano yaliyopangwa huku chanzo kutoka kwa kampuni ya mawasiliano kililiambia shirika la habari la Reuters kwamba amri ya kufunga mawasiliano ilitoka kwenye shirika la kitaifa la mawasiliano la Sudan.
Maandamano ya leo yanaadhimisha siku ya 11, ya maandamano makubwa tangu mapinduzi ya Oktoba 25, ambayo yalishuhudia kuondolewa na kisha kurejeshwa kwa Waziri Mkuu Abdalla Hamdok. Waandamanaji hao wamedai kuwa wanajeshi hawana jukumu lolote katika serikali wakati wa mpito kuelekea uchaguzi huru. Madaraja mengi ya kuelekea Khartoum yamefungwa na angalau mawili kati yao yamezuiwa na kontena za usafirishaji, mashahidi wa shirika la habari la Reuters walisema.