Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia, imesema nchi hiyo itaanza majaribio ya uzalishaji wa umeme katika bwawa lenye utata la Grand Rennaissance wakati wa msimu ujao wa mvua.
Wakati huohuo Ethiopia imesema itakuwa ikijiandaa kwa awamu ya pili ya kujaza maji kwenye bwawa hilo.
Taarifa ya wizara hiyo imesema hakuna chochote kinachoweza kuvuruga juhudi zinazoendelea za kujaza bwawa hilo wala mchakato wa utekelezaji wa mradi huo.
Misri na Sudan ambazo zinategemea rasilimali za maji ya mto Nile zimekuwa zikisisitiza haja ya makubaliano ya mwisho kuhusu bwawa hilo.
Mazungumzo juu ya bwawa hilo, ambayo yalianza mnamo mwaka wa 2011, wakati lilipoanza kujengwa yamekwama mara kadhaa, na kupelekea mvutano mkubwa wa kikanda.