Shutuma hizo zilitolewa wakati wa kuanza kwa awamu ya pili ya mazungumzo yalioanza Jumatatu kuhusu namna Ethiopia itakavyojaza bwawa hilo.
Sudan na Misri zina hofu kwamba mradi wa Ethiopia wa kuzalisha umeme, ambao umegharimu kiasi cha dola bilioni 4, unaweza kusababisha upungufu mkubwa wa maji kwenye mto Nile, nchini mwao.
Blue Nile ni tawi la mto Nile ambao Misri inategemea kupata asilimia 90 ya maji kwa watu wake milioni 100.
Mazungumzo ya karibu mwongo mmoja yamekosa kufikia makubaliano, namna Ethiopia inastahili kutumia maji ya mto huo huku ikijali maslahi ya Misri na Sudan.
Bwawa hilo la Grand Renaissance lipo umbali wa kilomita 15 kutoka mpaka wa Ethiopia na Sudan kwenye mto Blue Nile, ambao unabeba maji mengi hadi kwa mto Nile wenyewe, baada ya kukutana na White Nile, nchini Sudan.
Wiki iliyopita, Ethiopia, ambayo inasisitiza kwamba inahitaji bwawa hilo ili kuzalisha umeme wa kutosha kwa ukuaji wa uchumi, ilisema kwamba tayari imeshajaza kiwango cha maji kinachohitajika kutokana na mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha nchini humo.
Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba Ethiopia imekiuka makubaliano ya awali ya kutojaza bwawa hilo kabla ya kufanyika mazungumzo.
Hadi tukiandaa ripoti hii, Ethiopia haikuwa imejibu madai ya Misri na Sudan.
Kati ya masuala muhimu yatakayojadiliwa kwenye mkutano huo unaoongozwa na umoja wa Afrika ni namna bwawa hilo litakavyofanya kazi wakati wa kiangazi au kama hakuna mvua ya kutosha, na iwapo makubaliano yatakayofikiwa yatatambuliwa kisheria.
-Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC