Ethiopia kuwaachia wafungwa kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona

Waziri Mkuu Abiy Ahmed

Ethiopia inajiandaa kuanza kuwaachia zaidi ya wafungwa 4,000 Alhamisi, katika juhudi za kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Mwanasheria Mkuu Adanech Abebe amesema wafungwa walio hukumiwa kwa makosa ya jinai madogo madogo, ambayo yamebakiza kifungo cha chini ya mwaka mmoja, na wanawake wenye watoto, wanastahiki kuachiwa.

Ethiopia pia inawasafirisha wafungwa ambao ni raia wa kigeni walioshtakiwa kwa makosa ya usafirishaji wa dawa za kulevya kurudi makwao.

Hadi sasa, Ethiopia imethibitisha kuwepo maambukizi 12 ya virusi vya corona, na kutokana na kusambaa kwa haraka kwa virusi hivi katika bara la Afrika, serikali imeamua kuchukua hatua kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.

Hivi sasa, Waziri Mkuu Abiy Ahmed anawataka raia wa Ethiopia kushikamana na suala la kujitenga, pamoja na kuwepo makundi ya watu wanaopuuzia tahadhari hiyo na kukusanyika katika shughuli mbalimbali katika mji huo mkuu wa Addis Ababa.