Hata hivyo waziri mkuu hataanza kazi mara moja, kwa mujibu wa taarifa ya ofisi yake, ikiongeza kuwa ataendelea kusubiri ili apate nafuu zaidi akiwa nyumbani kwake.
Johnson alikuwa amelazwa hospitali ya St. Thomas mjini London wiki moja iliyopita, siku kumi baada ya vipimo kuonyesha ana virusi vya corona.
“Bado sitakuwa nimewashukuru madaktari na wauguzi vya kutosha, wameokoa maisha yangu,” Johnson aliwaambia wafanyakazi wa huduma ya afya ya taifa katika hospitali hiyo Jumapili – ikiwa ni kauli yake ya kwanza kutoa tangu alipopelekwa katika kitengo cha watu mahtuti.
Wakati Johnson akiendelea kupata nafuu, waziri wa mambo ya nje Dominic Raab amekuwa akikaimu nafasi ya uwaziri mkuu.
Katika salamu kadhaa kwenye mitando ya jamii, ofisi ya waziri mkuu iliyoko Downing Street imewatakia Waingereza Jumapili ya Pasaka njema ikiwakumbusha kuwa makanisa yataendelea kufungwa na amri ya kutotoka majumbani itaendelea kutekelezwa.
Wakati huohuo Uingereza inakabiliwa na makadirio ya kusikitisha kwamba inawezekana ikawa iliyoathiriwa vibaya zaidi na virusi vya corona katika bara la Ulaya.
Idadi ya vifo Uingereza imefikia 9,875 hadi kufikia wikiendi ambapo watu 900 walikufa siku ya Jumamosi.