Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 11:32

Tanzania, Kenya zaripoti maambukizi zaidi ya Covid-19


Mhudumu wa afya amfanyia vipimo vya joto raia mmoja wa Tanzania kwenye mpaka wa nchi hiyo na Kenya mjini Namanga.
Mhudumu wa afya amfanyia vipimo vya joto raia mmoja wa Tanzania kwenye mpaka wa nchi hiyo na Kenya mjini Namanga.

Tanzania Ijumaa ilitangaza maambukizi zaidi ya virusi vya Corona, watu watano wakiwa wamethibithishwa kuambukizwa jijini Dar-es-Salaam.

Hiyo inaifanya idadi ya watu waliombaukizwa virusi hivyo katika taifa hilo la Afrika Mashariki kufikia 32. Taarifa ya wizara ya afya ilieleza kwamba wote ni raia wa nchi hiyo.

Watu watatu wamekufa Tanzania kutokana na maambukizi ya virusi hivyo vinavyosababisha mgonjwa kuwa na shida ya kupumua.

Wizara hiyo ilisema kwamba wote waliopoteza Maisha yao ni wanaume.

Kufikia Ijumaa, wagonjwa 24 walikuwa wanaendelea kupata matibabu huku watu wawili wakipata nafuu na kuruhusiwa kuondoka hospitalini.

Taarifa hiyo aidha ilieleza kwamba wagonjwa wapya wote ni wanaumme wenye umri wa kati ya miaka 35 na 68.

Kenya nayo iliripoti visa 5 zaidi vya Covid-19 siku ya Ijumaa.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo imetangaza maambukizi mapya ya watu wawili na kufikisha idadi ya wote walioambukizwa kuwa tisa.

Nchini Botswana wabunge 57 waliwekwa karantini ya lazima kwa muda wa siku 14 baada ya muuguzi katika majengo ya bunge kuambukizwa virusi vya Corona.

Amri ya wabunge kuwekwa karantini ilitolewa na mkurugenzi wa huduma za afya nchini humo Malaki Tshipayagae.

Kufikia Alhamisi, Botswana ilikuwa imerekodi visa saba vya maambukizi mapya.

Kati ya waliogunduliwa kuambukizwa ni mhudumu wa afya aliyekuwa kazini katika majengo ya bunge wakati vikao vya bunge vilikuwa vinaendelea.

Nchini Afrika kusini, Rais Cyril Ramaphosa aliongeza muda wa watu kusalia majumbani mwao kwa wiki mbili zaidi hadi mwishoni mwa mwezi Aprili.

Muungano wa wafanyakazi wa Afrika kusini umeondoa kesi mahakamani uliyokuwa umewasilisha dhidi ya serikali kuhusiana na uhaba wa vifaa vya matibabu na vya kujikinga dhidi ya hatari ya maambukizi kwa ajili ya madaktari na wauguzi

Nchini Kenya, Gavana wa Mandera Ali Roba aliamuru watu kusalia makwao baada ya watu wawili kugunduliwa kuwa na virusi hivyo hatari katika kaunti hiyo.

Zaidi ya watu 30 wamewekwa karantini katika kaunti ya Mandera, huku juhudi zikiendelea kuwatafuta watu waliokaribiana na wagonjwa ambao wamelazwa katika hospitali kuu ya Kaunti hiyo.

Gavana Roba alisema nchi ambazo zimepata mafanikio katika vita dhidi ya virusi vya Corona ni zile zinazotekeleza amri ya watu kusalia nyumbani kwao ili kuzuia maambukizi.

Kufikia wakati wa kuandaa ripoti hii, Kenya ilikuwa imerekodi visa 189 vya maambikizi ya Corona, vifo 7 na watu 12 kupata nafuu na kuruhusiwa kuondoka hospitalini.

-Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG