Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 01:17

Viongozi wa Afrika wamkosoa Trump kwa kutaka kusitisha msaada kwa WHO


Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika Mousa Faki Mahamat
Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika Mousa Faki Mahamat

Baadhi ya viongozi barani Afrika wameeleza kushangazwa kwao na tamko la rais wa Marekani kwamba anafikiria kusitisha msaada wa kifedha kwa Shirika la Afya Duniani WHO.

Viongozi hao wametoa wito kwa Marekani kuweka kando siasa kwa sasa na badala yake kuungana mkono katika kupambana na janga la maambukizi ya Virusi vya Corona.

Wito huo umetolewa baada ya rais wa Marekani Donald Trump kusema kwamba utawala wake unatafakari hatua ya kutoendelea kutoa msaada wa kifedha kwa shirika la afya duniani WHO, akilishitumu kwa "kupendelea China katika vita dhidi ya Corona."

Katika ujumbe wa Twiter, mweyekiti wa umoja wa Afrika AU, Moussa Aki Mohamat, amesema kwamba ameshtushwa sana na kampeni ya serikali ya Marekani dhidi ya shirika la afya Duniani WHO.

“Umoja wa Afrika unaunga kwa dhati juhudi za WHO katika kupambana na virusi vya Corona na kutaka viongozi wote wa dunia, kuungana katika kuzuia maambukizi na vifo kutokana na virusi hivo” ameandika Mahamat kwenye mtandao huo.

Rais wa Rwanda Paul Kagame naye kwa kutumia ujumbe wa twitter, amesema anakubaliana na matamshi ya mwenyekiti wa umoja wa Afrika ya kutaka ushirikiano katika kuangamiza maambukizi ya virusi vya Corona.

“Inasikitisha kwamba nchi kadhaa duniani na mashirika mbalimbali, ikiwemo Marekani, China na shirika la afya duniani, yanakabiliwa na tishio la maambukizi ya Corona. Hakuna haja ya viongozi kuanza kuashambulia wengine au shirika lolote kwa sasa,” ameandika Kagame.

Kagame, ametaka viongozi kuweka kando siasa kwa sasa, na kuangazia jinsi ya kuangamiza virusi hivyo hatari, akimalizia ujumbe wake wa twiter kwa kauli kwamba Afrika haitaki siasa zinazoanza kujitokeza kwa sasa kuhusiana na ni nani anastahili kuwajibika kwa kufanya nini kutokana na janga la virusi vya Corona.

Rais Donald Trump ametishia kuafutilia mbali msaada wa kifedha kwa shirika la afya duniani, akidai kwamba shirika hilo linapendelea China.

"Shirika la afya duniani kupokea kiasi kikubwa cha pesa kutoka kwa Marekani. Tumewapatia zaidi ya dola milioni 58. Walikosoa na kukataa mpango wangu wa kuweka marufuku kwa safari kuingia na kutoka nchini. Walifanya makosa, na wamekuwa wakifanya makosa kila mara. Walipata taarifa mapema kuhusu maambukizi ya Corona. Wanaonekana kupendelea sana China. Hilo ni jambo ambalo tunastahili kufuatilia sana,” amesema Trump.

Awali, kabla ya kusema hayo katika kikao na waandishi wa habari, Trump alishambulia shirika la WHO kupitia ujumbe wa twiter, akilishutumu kwamba linapendelea sana kusifia jinsi China imeshughulikia janga la maambukizi ya Corona.

Trump anadai kwamba China ilitoa habari za uongo kwa Marekani, na kupelekea kuendelea kufungua mipaka yake kwa wasafiri kutoka China.

Hadi tukitayarisha ripoti hii, Shirika la afya duniani halikuwa limetoa taarifa kujibu matamshi na vitisho vya Trump.

Kwingineko kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis ameshutumu kile ametaja kama watu wanaotumia janga la maambukizi ya Corona kujibinafsisha kibiasashara.

“Baadhi ya wanasiasa wamejaa unafiki, kutokana na jinsi wanavyoshughulikia janga la Corona,”amesema Papa Francis wakati wa misa mjini Vatican.

Francis, amewaomba watu wanaojifaidisha kutokana na Corona, kubadili mioyo yao na kutenda yaliyo ya haki kwa binadamu na kwa mwenyezi mungu, akiomba Mungu kubadilisha mioyo na nafsi zao.

Jumla ya watu 83, 471 wameaga dunia kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona kote duniani, kufikia wakati tunaandaa ripoti hii.

Kufikia sasa, maambukizi zaidi yanaripotiwa nchini Marekani, kuliko nchi yoyote ile duniani, watu 399, 929 wakiwa wameambukizwa na vifo vya watu 12911 kuripotiwa.

Maambukizi na vifo yanaendelea kuripotiwa katika nchi kadhaa za Afrika.

-Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA Washington DC

XS
SM
MD
LG