Biden aendelea kuongoza Pennsylvania dhidi ya Trump

Rais Donald Trump na Makamu wa Rais Joe Biden.

Kuongoza katika kura kwa mgombea wa Chama cha Demokratik Joe Biden dhidi ya Rais wa Marekani Donald Trump katika jimbo la Pennsylvania kumeongezeka kutoka kura 5,000 mapema Ijumaa kufikia kura 29,000 usiku wa Ijumaa, ongezeko hilo linatarajiwa kukua wakati kura zilizosalia zikiendelea kuhesabiwa.

Kushinda katika jimbo hili muhimu kutamuwezesha Biden kufikia kiwango cha kura 270 za wajumbe zinazohitajika ili kushinda uchaguzi wa rais.

Biden pia anaongoza huko Georgia kwa zaidi ya kura 4,000, na ameendelea kuwa na uongozi wa waziwazi Arizon na Nevada, japokuwa uchaguzi huu haujatangaza nani mshindi kwa wagombea wote wawili.

Akiwahutubia wafuasi wake Ijumaa, katikati ya ubashiri kuwa atatangazwa mshindi huko Pennsylvania, Biden alijizuia kujitangazia ushindi.

“Hatuna tamko la mwisho la aliyeshinda mpaka sasa, lakini hesabu inatuambia wazi, ni habari yenye kutia moyo, tutashinda uchaguzi huu,” Biden amesema.

Iwapo Biden atashinda Pennslyvania, Kura za Wajumbe anazoongoza zitaongezeka kufikia kura 273 dhidi ya jumla ya kura za Trump za sasa 214.

Ushindi wa Biden huko Pennsylvania pia utamzuia Trump kuelekea kupata ushindi.

Trump anaongoza katika majimbo mawili ya North Carolina na Alaska ambayo bado hayatangaza matokeo. Bila ya kushinda Pennsylvania, Trump hawezi kumpiku Biden hata kama atashinda majimbo mengine yote ambayo hayajamaliza kuhesabu kura.

Biden amemshinda Trump kwa kura milioni 4 katika uchaguzi wa taifa. Biden ameshinda zaidi ya kura milioni 74 dhidi ya kura za Trump milioni 69, wakati zaidi ya kura milioni 150 zimepigwa nchi nzima, idadi kubwa zaidi ambayo haijawahi kutokea katika historia ya uchaguzi wa Marekani.