Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 01:21

Wamarekani wanasubiri kujua nani atashinda urais


Rais Donald Trump kushoto and Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden
Rais Donald Trump kushoto and Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden

Huenda Wamarekani wakakesha Jumatano kabla ya kujua nani atakuwa rais wao mpya kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo kwenye uchaguzi huu uliofanyika wakati taifa hili limegawika sana kwa mara ya kwanza tangu vita vya Vietnam miaka 1970.

Kura zinahesabiwa katika majimbo yote hivi sasa na katika majimbo ya mashariki inaonekana wagombea hao wawili wanapata ushindi katika ngome zao za kawaida wakati ushindani uko katika majimbo mengi na imekuwa vigumu kutabiri nani atapata ushindi.

Hapa Marekani ushindi unategermea zaidi katika majimbo kwani kila mmoja anagombania wajumbe wa majimbo hayo kuweza kushinda uchaguzi. Kuweza kupata ushindi mgombea kiti cha rais anahitaji kupata kura 270 za wajumbe wa majimbo.

Chanzo cha VOA wakati tunachapisha habari hizi kilikuwa kinaonyesha Biden anaongoza akiwa na kura 205 za wajumbe wa majimbo na Trump ana 100.

Kwa upande wa Baraza la Senate kila kipindi cha uchaguzi theluthi moja tu ya viti vinashindaniwa hivyo kuna viti 35 vinagombania na wademokrat wanahitaji viti vitatu au vinne zaidi kuchukua udhibiti kutoka wa Republikan.Mbali na mashindano hayo ya kiti cha rais kuna mashindano ya wajumbe wa Bunge Kuu la Marekani ambao wabunge wote 435 wa baraza la wawakilishi au baraza kuu la bunge wanagombea kiti, lakini wachambuzi wanasema Wademokrats wataendelea kulidhibiti baraza hilo wakiongeza viti vitano.

Bunge la Marekani
Bunge la Marekani

Katika uchaguzi huu kuna viti saba vinavyoshikiliwa na Warepublican vyenye ushindani mkubwa na utafiti unaonyesha huenda Wademokrat wakanyakua baadhi ya viti hivyo hadi sasa wamenyakua kiti kimoja zaidi.

Uchaguzi huu unachukuliwa wa kihistoria kutokana na idadi ya watu walioshiriki ambapo watu milioni 100 walipiga kura mapema au kwa njia ya posta na zaidi ya milioni 150 wamepiga hiyo jana.

Katika baadhi ya majimbo karibu asilimia 90 ya walioandikishwa walipiga kura na kudhihirisha kwamba uchaguzi huu ulikuwa muhimu lakini mwaka huu masuala ya uchumi na sera hayakuchukua nafasi ya juu, badala yake Biden aliongoza kampeni yake kuhusiana na janga la Corona.

Biden alijikita katika suala la corona akimlaumu Trump alivyoshughulikia janga hili na Marekani kuwa na idadi kubwa ya vifo duniani.

Warepublikan kwa upande wao wamezingatia hali ya Uchumi na usalama hasa kutokana na ghasia zilizo sababiswa na unyanyasaji wa polisi dhidi ya Wamarekani weusi. Kwa hivyo huenda tusijuwe nani mshindi wa uchaguzi wa Marekani hadi baadae mchana Jumatano.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC

XS
SM
MD
LG