Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 08:43

Mmarekani mweusi wa asili ya Kenya agombea udiwani Minnesota


Henry Momanyi
Henry Momanyi

Henry Momanyi, Mmarekani mweusi wa asili ya Kenya, anagombea kiti cha udiwani katika mji wa Brooklyn Park, eneo wakilishi la West District, jimbo la Minnesota kwa tikiti ya chama cha Demokratik.

Momanyi, mwenye umri wa miaka 51, anagombea nafasi inayoshikiliwa na Diwani Susan Pha wa chama cha Republikan, anayewania tena katika uchaguzi wa mwaka huu utakaofanyika Jumanne tarehe tatu mwezi Novemba mwaka huu.

Wanasiasa hao wawili walishinda tikiti za vyama vyao kwenye uchaguzi wa awali na kuteuliuwa na vyama hivyo mapema mwaka huu.

Katika mahojiano na idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika, Momanyi amesema ana matumaini makubwa ya kupata ushindi kwa sababu amepata uungwaji mkono na wakazi wengi wa mji huo, wakiwa ni pamoja na wahamiaji kutoka bara la Afrika.

“Hapa watu wananiunga mkono bila kujali rangi. Nawashukuru sana Waafrika wenzangu hususan kutoka Afrika Mashariki na Magharibi kwa kusimama na mimi wakati huu wa kampeni hata ingawa hii ni mara yangu ya kwanza kugombea,” alisema.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo chipukizi amesema anakabiliwa na changamoto za ufadhili wa kampeni yake.

“Tuna changamoto za kifedha kwa sababu hatujapata uidhinishwaji kama ilivyo kwa wanasiasa wengine waliobobea. Hiyo ina maana kwamba hatuna hela za kutosha kufadhili kampeni yetu. Lakini tunajitahidi na kumtanguliza Mungu,” alisema Momanyi.

Mzaliwa wa jimbo la Kisii nchini Kenya, Momanyi alihamia Marekani mnamo mwaka wa 1998 akiwa na umri wa miaka 28.

Anasema baada ya kumaliza masomo yake, amefanya kazi ya kuhamasisha masuala ya kijamii kwa Zaidi ya miaka ishirini kabla ya kuamua kuwania nafasi ya kisiasa.

“Nimeona changamoto nyingi wanazopitia wakazi wa jimbo hili, ikiwa ni pamoja na makazi, usalama, elimu na hali duni ya mawasiliano kati ya wakazi na maafisa wa baraza la mji huu,” amesema.

Mgombea huyo ni mmoja wa wahamiaji kadhaa kutoka bara la Afrika ambao wanawania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa Marekani wa mwaka 2020.

Momanyi na familia yake - mkewe Jeliah Momanyi na watoto wao watatu -wanaishi katika mji huo wa Brooklyn Park.

XS
SM
MD
LG