Hata hivyo hakukuwa na taarifa za papo hapo zinazothibitisha kuwa nchi hizo tano zilikuwa zimepokea rikodi hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema mapema wiki hii serikali yake inazo taarifa zaidi kuhusiana na mauaji haya na kuna uwezekano mkubwa itaweka hadharani ushahidi huu baada ya uchunguzi wa kifo cha Khashoggi kukamilika.
Akizungumza wakati wa ziara yake Japan, Cavusoglu amewaambia waandishi wa habari kuwa Uturuki imesema Saudi Arabia na nchi nyingine ambazo zina maslahi na ripoti hizi wamepewa fursa ya kuziona.
Khashoggi aliuwawa katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia huko mjini Istanbul Octoba 2.
Hapo awali, Saudi Arabia ilisema Khashoggi alikuwa ameingia katika ubalozi huo na kuwa taarifa za alikokwenda hazijulikani, lakini baadae walisema alikufa katika mapigano ya kurushiana ngumi na hatimaye wakasema alikufa kwa kupigwa kabari.
Mwendesha mashtaka wa Ufalme huo tangu wakati huo ameyaita mauaji hayo yalipangwa, lakini hakueleza nani aliyekuwa ameyapanga au kuyaidhinisha.