Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 00:04

Ukraine yaomba 'kupewa msaada wa juu' kuzuia madhara ya kiuchumi Ulaya


Dmytro Kuleba
Dmytro Kuleba

Ukraine imetoa wito Jumatatu “kupewa msaada wa juu” kwa juhudi zake za kuishinda Russia ili kuzuia madhara ya kiuchumi kwa washirika wa Ulaya, wakati Russia ikirejea kulaumu vikwazo vya Magharibi vilivyosababisha matatizo ya usafirishaji wa mafuta  kwenda Ujerumani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba alisema “uchokozi wa kijeshi dhidi ya Waukraine, usaliti wa nishati dhidi ya raia wa EU” unaofanywa na Russia ndiyo wakulaumiwa kwa “ongezeko la bei na gharama za matumizi katika nchi za EU.”

“Suluhisho: msaada wa juu kwa Ukraine ili tuweze kumshinda Putin haraka iwezekanavyo na asiweze kuidhuru Ulaya tena,” Kuleba alitweet.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliwaambia waandishi kuwa vikwazo vya Magharibi vilikuwa “vinasababisha matatizo” kuweza kukarabati bomba la Nord Stream 1, ambalo kampuni kubwa ya nishati ya Russia, Gazprom ililifunga wiki iliyopita ikisema imebaini kuwa mafuta yanavuja.

Nchi za Ulaya ambazo zimepeleka silaha kadhaa kwa serikali ya Kyiv na kuwapa mafunzo wapiganaji wake zimeishutumu Russia kutumia usambazaji wa nishati waliyonunua kutoka Moscow kama silaha.

“Matatizo ya usambazaji wa gesi yamejitokeza kwa sababu ya vikwazo vilivyowekwa na nchi za magharibi kwa nchi yetu, ikiwemo Ujerumani na Uingereza,” Peskov alisema.

Kundi la nchi tajiri zaidi duniani (G7) zimependekeza kuweka kiwango cha bei kwa mafuta yanayouzwa na Russia ili kudhibiti faida inayopata Russia ambayo inasaidia kudhamini juhudi za vita vya Russia huko Ukraine.

Russia, nayo imejibu, itaacha kuuza mafuta kwa nchi yoyote itakayo weka kiwango cha bei kama hicho.

Chansela wa Ujerumani Olaf Scholz aliahidi Jumapili kuwa Ujerumani itafanikiwa kukabiliana na hali hii wakati wa baridi, akiuambia mkutano wa waandishi mjini Berlin, “Russia imesita kuwa mshirika wa kutegemewa katika nishati.”

Scholz alitangaza mpango wa unafuu wa dola bilioni 65 ambao unajumuisha malipo ya mara moja kwa kila kaya, nafuu ya kodi kwa viwanda ambavyo vinatumia kiwango kikubwa cha mafuta na fursa za usafiri wa umma wa bei nafuu.

Serikali ya Berlin pia imepanga kudhamini raia wake kiwango fulani cha umeme cha bei ya chini zaidi.

Baadhi ya taarifa za habari hii zinatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.

XS
SM
MD
LG