Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:08

Trump atangaza hakuna karantini New York, Connecticut na New Jersey


Donald Trump akiongea na waandishi wa habari wakati kabla ya kuondoka kuelekea Norfolk, Virginia, Machi 28, 2020. REUTERS/Joshua Roberts.
Donald Trump akiongea na waandishi wa habari wakati kabla ya kuondoka kuelekea Norfolk, Virginia, Machi 28, 2020. REUTERS/Joshua Roberts.

Rais wa Marekani Donald Trump amebadilisha kauli yake ya kufikiria kuamrisha karantini kudhibiti maradhi yanayotokana na virusi vya corona katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi ya New York, New Jersey na Connecticut, na badala yake ameamrisha Jumamosi usiku kuwa “ushauri makini wa kusafiri” utolewe ili kuzuia kuenea kwa mlipuko huo.

Makamu wa Rais Mike Pence alituma ujumbe wa Twitter akisema Kituo cha Kuzuia Maradhi (CDC) kinawataka wakazi wote wa majimbo hayo matatu “kutofanya safari ambazo siyo muhimu kwa kipindi cha siku 14 zijazo.

Fikra ya karantini ilikuwa imehamasishwa na magavana kadhaa, akiwemo Ron DeSantis wa Florida (Mrepublikan) ambaye alitaka kuzuia wasafiri kutoka maeneo yaliyoathirika zaidi kuingia katika majimbo yao. Lakini hilo lilikosolewa mara moja na viongozi wa majimbo hayo yanayojadiliwa, ambao walitahadharisha itasababisha wasiwasi katika jamii ambayo tayari inaadhibika kutokana na virusi hivyo.

Trump alitangaza kufikia uamuzi huo baada ya kushauriana na kikundi kazi cha White House kinachoongoza harakati za Serikali kuu za kukabiliana na mlipuko wa corona na magavana wa majimbo hayo matatu. Amesema alikuwa amewaagiza CDC “ Kutoa ushauri makini wa kusafiri utakaosimamiwa na magavana, wakishauriana na serikali kuu.”

Aliongeza kuwa : Karantini haitahitajika.”

Gavana Andrew Cuomo wa New York, ambaye amekosoa serikali kuu inavyokabiliana na maradhi hayo wakati jimbo lake likiwa ni chimbuko la maambukizi nchini, amesema kuyatenga majimbo itakuwa sawa na “serikali kuu kutangaza vita.”

Cuomo amesema suala la uwezekano wa kuwepo karantini hazikujadiliwa wakati wa mazungumzo yake na Trump mapema Jumamosi, akiongeza kuwa anaamini itakuwa ni kinyume cha sheria, balaa la kiuchumi, “upuuzi” na upeo mdogo wakati maeneo mengine ya Marekani yanashuhudia kuongezeka kwa maambukizi hayo pia.

“Ukianza kuyatenga maeneo kadhaa kote nchini (Marekani), itakuwa ni maajabu kabisa, haitakuwa na tija, ni dhidi ya Umarekani, na kinyume na mshikamano wa kijamii,” Cuomo amekiambia kituo cha habari cha CNN.

Alisema kuyatenga makao makuu ya kiuchumi ya taifa (New York) utaleta mtikisiko katika soko la hisa na “kudhoofisha uchumi” wakati ambao Trump ameeleza anahangaika kurejesha hali ya uchumi mahali pake nchini.

Trump alitoa kauli yake ya awali alipokuwa yuko njiani kuelekea mji wa Norfolk, Virginia, kushuhudia kuondoka kwa meli ya jeshi la majini ambayo ni hospitali ikielekea jijini New York kusaidia kukabiliana na mlipuko wa janga la corona.

Katika tukio hilo, alizungumza na kundi dogo lililokuwa katika kituo hicho cha kijeshi na kuwatahadharisha kuchukua hatua za kujikinga, japokuwa yeye mwenyewe, umri wake miaka 73, ni katika kundi lenye uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi na ni kati ya wale walioshauriwa kujiepusha na safari ambazo sio muhimu.

Serikali kuu inajukumu la kuchukua hatua kuzuia kuenea kwa maradhi ya maambukizi kati ya majimbo, lakini haiko wazi hiyo inamaanisha kuwa Trump anaweza kuzuia watu kuondoka kutoka katika majimbo yao.

Amri kama hii haijawahi kujaribiwa katika zama hizi – na kwa matukio machache wakati karantini ilipopingwa, mahakama kwa ujumla zilikubaliana na maamuzi ya maafisa wa afya ya umma.

Mahakama zimetoa uamuzi uliojirejea kwa miaka kadhaa kwamba mamlaka ya kuamrisha karantini katika majimbo ni la uongozi wa majimbo hayo kwa ujumla, chini ya vifungu vya Katiba za kujitawala na sio wazi iwapo zimetolewa kwa serikali kuu kuyaamulia majimbo.

Serikali kuu, hata hivyo, itakuwa na mamlaka chini ya vifungu vya katiba vinavyosimamia biashara kuweka karantini dhidi ya wasafiri wa kimataifa au wale wanaosafiri kutoka jimbo hadi jimbo ambao huenda wakawa wanapeleka magonjwa hatarishi.

Bado, “ni jambo halijawahi kutokea kabisa kwamba gavana au rais atawazuia watu kusafiri kutoka jimbo moja kwenda jimbo jingine wakati wa mlipuko wa maradhi ya maaambukizi,” amesema Lawrence Gostin, Mhadhiri wa Sheria na mtaalam wa afya ya umma wa Chuo Kikuu cha Georgetown aliyedadisi uwezo wa Trump kuamrisha karantini dhidi ya majimbo.

Lakini wakati Trump akielekea Norfolk, alituma ujumbe wa Twitter : “Ninafikiria kuanzisha karantini katika maeneo yanayoendelea kuwa “hatarishi zaidi”, New York, New Jersey, na Connecticut. Uamuzi utafikiwa, kwa njia moja au nyingine, muda sio mrefu.”

“Majimbo mengi ambayo yanamaambukizi lakini hayana tatizo kubwa la ugonjwa huo, wameniuliza iwapo nitaweza kulifikiria jambo hilo, na hivyo tutaliangalia,” Trump amesema.

Alipoulizwa juu ya amri ya kutangaza karantini kisheria, mkuu mpya wa wafanyakazi wa White House, Mark Meadows, amesema maafisa “wanatathmini yote yanayowezekana kufanyika hivi sasa.”

XS
SM
MD
LG