Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 21:53

Kenya: Watu saba zaidi waambukizwa Corona huku marufuku ya kutoka nje ikiibua utata


Waziri wa Afya wa Kenya, Mutahi Kagwe.
Waziri wa Afya wa Kenya, Mutahi Kagwe.

Wizara ya Afya ya Kenya ilisema Jumamosi kwamba idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya Korona imeongezeka na kufikia 38. Hii ni baada ya watu wengine saba kupatikana na virusi hivyo baada ya kufanyiwa vipimo.

Wagonjwa waliobainika kuwa na virusi hivyo hatari ni wanaume watatu na wanawake wanne. Wanne kati yao ni raia wa Kenya, wawili wa asili ya Congo na mmoja raia wa Uchina.

Maafisa wa Wizara ya Afya walivieleza vyombo vya habari Jumamosi kuwa saba hao walikuwa miongoni mwa watu wengine 81 waliofanyiwa vipimo vya afya katika kipindi cha saa ishirini na nne.

"Wanne kati ya hawa saba wana historia ya kusafiri kutoka mataifa yalio na maambukizi. Mmoja alisafiri kutoka Mombasa lakini wawili hawana historia ya kusafiri nje," alieleza waziri wa Afya, Mutahi Kagwe.

Kagwe pia alisema kuwa matokeo ya pili ya vipimo vya afya ya mgonjwa wa kwanza na wa tatu kutambulika na virusi vya Corona yanaonyesha kutokuwa na dalili za maambukizi. Sampuli za vipimo hivyo zimechukuliwa katika kipindi cha saa ishirini na nne.

Aidha waziri huyo alifafanua kuwa vipimo vingine vitafanywa katika kipindi cha saa 48 zijazo kuthibitisha hali kamili.

"Hii ni ishara nzuri kwa sababu wameonesha ishara za kupona na wanaendelea vizuri," aliongeza.

Kufikia Jumamosi asubuhi Kenya ilikuwa imerekodi kisa kimoja cha kifo kutokana na virusi vya Corona, cha mwanamume wa miaka 66 aliyefariki akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Aga Khan, jijini Nairobi.

Maafisa wa afya walfichua kuwa jimbo la jiji la Nairobi linaongoza kwa wagonjwa 28, Kilifi wagonjwa 6, Mombasa wagonjwa 2, Kwale na Kajiado mgonjwa mmoja kila jimbo.

Aidha, Waziri Kagwe alieleza kuwa jumla ya watu 883 wamechunguzwa na kufanyiwa vipimo vya afya. Wengine zaidi ya 1,000 walitajwa kutangamana na wagonjwa wanaolazwa katika hospitali ya Mbagathi jijini Nairobi.

Kuanzia Ijumaa, serikali ya Kenya ilianza kutekeleza katazo la kutoka nje kuanzia saa moja machweo na saa kumi na moja macheo kila siku ili kudhibiti ueneaji zaidi wa virusi vya Corona.

Hata hivyo, katazo hilo limeshtumiwa na raia mbalimbali wa Kenya baada ya maafisa wa polisi kunaswa kwenye runinga nchini humo wakitumia nguvu kupita kiasi, viboko na gesi za kutoza machozi kuwafukuza waliojipata nje.

Afisa wa Polisi alinaswa kwenye runinga akimhangaisha mwanahabari wa shirika la habari la Nation Media mjini Mombasa Peter Wainaina saa chache kabla kipindi cha katazo hilo kufika.

Pia, raia wengine kwenye kivuko la Likoni walilazimishwa kulala chali palipo na vidimbwi.

Kufuatia hilo, rais wa baraza la wanasheria nchini Kenya, LSK, Nelson Havi aliishtumu vikali hulka hiyo ya baadhi ya maafisa wa polisi.

"Baraza la Wanasheria nchini Kenya litaelekea mahakamani Jumatatu kupinga katazo hili linalotekelezwa kinyume cha sheria na ambalo limetumiwa vibaya na maafisa wa polisi.

Ni dhahiri kuwa Virusi vya Corona vitasambaa zaidi kutokana na matendo ya maafisa wa polisi kuliko wote wanaokaidi katazo hili," alieleza Nelson Havi.

-Imetayarishwa na Mwandishi wa VOA Kennedy Wandera, Nairobi, Kenya

XS
SM
MD
LG