Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 05:00

Trump afunguliwa mashtaka kwa kutumia madaraka vibaya na kuzuia uchunguzi


Baraza la Wawakilishi likipiga kura wakati Spika wa Bunge Nancy Pelosi wa California, akiwa mbele yao. Kura hiyo ni kupitisha kifungu cha pili cha kumfungulia mashtaka ya kumuondoa madarakani Rais Donald Trump, Jumatano, Disemba 18, 2019, huko Bungeni, Washington. AP Photo/Patric
Baraza la Wawakilishi likipiga kura wakati Spika wa Bunge Nancy Pelosi wa California, akiwa mbele yao. Kura hiyo ni kupitisha kifungu cha pili cha kumfungulia mashtaka ya kumuondoa madarakani Rais Donald Trump, Jumatano, Disemba 18, 2019, huko Bungeni, Washington. AP Photo/Patric

Baraza la Wawakilishi Jumatano usiku limemkuta na makosa Rais Donald Trump kwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kujinufaisha yeye mwenyewe na pia kuzuia juhudi za bunge kuchunguza vitendo vyake.

Katika kura ambapo kila upande wa chama uliegemea upande wake, Baraza la Wawakilishi linalodhibitiwa na Wademokrat lilipitisha vifungu viwili vya kumshtaki Trump, Mrepublikan, na hivyo kufanya awe rais wa tatu wa Marekani kufunguliwa mashtaka katika historia ya miaka 243 ya nchi hii.

Trump ambaye amekejeli tuhuma za mashtaka yaliyo funguliwa kumuondoa madarakani na kuwashambulia Wademokrat kwa kushinikiza hilo, hivi sasa kuna uwezekano wakukabiliwa na kesi mwezi Januari 2020, katika Baraza la Seneti.

Lakini Warepublikan waliowengi katika Baraza la Seneti inatarajiwa zaidi kutomuondoa madarakani, na hivyo kuwaachia wapiga kura kuamua juu ya hatma yake Trump wakati akiomba muhula wa pili kurejea White House katika uchaguzi mkuu Novemba inayokuja.

White House imetoa tamko mara tu baada kupigwa kura, inayosema, “Leo ndiyo kilele cha tukio la kuaibisha la kisiasa katika Baraza la Wawakilishi katika historia ya taifa letu. Imesema hatua hiyo ni “mashtaka ya uongo.”

Tamko hilo limeongeza kusema, “Rais anayakini kuwa Baraza la Seneti litarejesha hali ya kawaida, yenye haki, na mchakato wa sheria, vyote hivyo vilipuuziwa katika mjadala wa Baraza la Wawakilishi. Yuko tayari kwa hatua zinazofuata na hana shaka kuwa atakutikana hana makosa kabisa.”

Baraza la Wawakilishi lilijadili faida za kumfungulia Trump mashtaka ya kumuondoa madarakani kwa zaidi ya masaa sita kabla ya kupiga kura. Wawakilishi wa chama cha Demokrat waliendeleza suala la kufunguliwa mashtaka Trump.

Walikinzana na Warepublikan, wanaosema kuwa Trump hakufanya makosa yoyote katika juhudi zake za kushinikiza kwa kipindi cha mwezi mzima Ukraine ichunguze mmoja wa mahasimu wa kisiasa wa Trump wa chama cha Demokrat katika uchaguzi wa mwaka 2020, shughuli za kampuni ya gesi yenye tija ya Makamu wa Rais Joe Biden, mtoto wake Hunter Biden, na nadharia iliyojitokeza kuwa Ukraine iliingilia kati uchaguzi mkuu wa 2016 ambao Trump alishinda, ili kuhujumu kampeni yake.

Trump alimtaka Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amchunguze Biden katika mazungumzo ya simu mwishoni mwa Julai wakati ambapo alikuwa amezuilia kwa muda msaada wa kijeshi uliokuwa umetolewa kwa ajili ya Kyiv wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 391 ambao mji wa Kyiv ulikuwa unataka utumike kusaidia kupambana na waasi wa nchi hiyo waliojitenga wanaosaidiwa na Russia huko Ukraine mashariki

Hatimaye Trump alitoa fedha hizo Septemba bila ya Zelenskiy kuanzisha uchunguzi dhidi ya Biden, hivyo Warepublikan walisema wakati wa majadiliano ndani ya Bunge kuwa ni ushahidi kwamba Trump alikuwa hajajihusisha na kitendo chochote cha kudai kufanyiwa fadhila na Ukraine kumchunguza Biden kama ni malipo ya msaada huo wa kijeshi.

Moja ya vifungu hivyo vya kumfungulia mashtaka kilichopitishwa na Baraza hilo kilimshutumu Trump kwa kutumia vibaya madaraka yake ya urais kwa kuomba fadhila kutoka serikali ya kigeni ya Ukraine, kufanya uchunguzi ili kumsaidia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi dhidi ya Biden, ambaye anaongoza katika kura za maoni za Wademokrat kitaifa katika uchaguzi wa kumtafuta mteule wa urais atakaye pambana na Trump mwaka 2020.

Madai ya shtaka la pili yalisema Trump alizuia maelfu ya nyaraka zinazohusiana na Ukraine kuwasilishwa kwa wachunguzi wa Baraza la Wawakilishi waliokuwa wanamchunguza ili kufungua mshtaka ya kumuondoa madarakani na kisha aliwazuia maafisa muhimu ndani ya uongozi wake kuja kuhojiwa wakati wa wiki za majadiliano yaliyokuwa yanaendeshwa na kamati zilizokua zimedhibitiwa na Wademokrat yakijikita katika vitendo vya Trump vinavyohusiana na Ukraine.

XS
SM
MD
LG