Fiona Hill ametofautiana na Rais Trump ambae anaonekana kuamini kauli ya rais Vladmir Putin aliekanusha tuhuma za Russia kuingilia kwenye uchaguzi wa 2016.
Katika mazungumzo ya simu ya Julai 25, Rais Trump alimuomba Rais wa Ukraine Volodomir Zelensky kuanzisha uchunguzi dhidi ya hasimu wake wa kisiasa aliyekuwa Makamu wa Rais Joe Biden, na kuchunguza iwapo kuna watu wa Ukraine walioshirikiana na mgombea wa chama cha Demokrat kwenye uchaguzi wa 2016, Hillary Clinton.
Hill amesema juhudi za afisa kwenye utawala wa Trump kutaka Ukraine ianzishe uchunguzi dhidi ya wapinzani wa Trump, ni mbinu za siasa ya ndani ambazo ni tofauti na malengo ya sera za nje za Marekani.
Hill ameongeza kuwa madai kwamba Ukraine iliingilia uchaguzi wa Marekani wa 2016 ni proganda za idara za usalama za Russia. Amewataka wanachama wa Kamati ya Upelelezi kujiepusha na siasa za uzushi ambazo zinaifaidisha Russia.
Wademocrat walio wengi kwenye Baraza la Wawakilishi walianzisha uchunguzi wa kumfungulia mashtaka ya kumuondoa madarakani Rais Trump, wakimshtumu kukiuka katiba ya Marekani na kutumia vibaya madaraka kwa kumuomba Rais wa kigeni kuingilia siasa za ndani za Marekani, kwa maslahi yake binafisi.
Trump na Warepublikan wanazidi kukanusha kwamba Rais wa Ukraine alishinikizwa, ili aweze kupata msaada wa kijeshi wa dola millioni 391 kutoka Marekani.
Wademokrat sasa wanasema wanao ushahidi wa kutosha wa kuonyesha kwamba Rais Trump alikiuka katiba ya nchi.