Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Novemba 24, 2024 Local time: 00:02

Je, Mwanasheria Mkuu Barr ni wakili wa Trump?


Rais Donald Trump
Rais Donald Trump

Mvutano wa kisiasa na kisheria watokota kati ya ikulu ya Marekani na Bunge jambo linalo sababisha wadadisi wa mambo kuhofia kuzuka kwa mzozo wa kikatiba ikiwa suluhisho halitapatikana haraka.

Kiini cha mzozo huo kilianza wiki hii pale Waziri wa Sheria alipokataa kufika mbele ya kamati ya sheria ya baraza la wawakilishi kutoa ushahidi kuhusu ripoti ya mwendesha mashtaka maalum kuhusiana na Rashia kuingilia kati uchaguzi wa Marekani.

Takriban miezi mitatu baada ya kuidhinishwa kuwa Waziri wa sheria na Mwanasheria Mkuu wa serikali, William Barr, ajikuta katika kizungumkuti ambacho alisema hataki kujihusisha nacho alipokuwa anahojiwa ili kupitishwa kuwa waziri.

Lakini baada ya kutoa ushahidi mapema mwezi Mei, mbele ya Kamati ya Sheria ya Baraza la Seneti ambalo linadhibitiwa na chama tawala cha Republikans naye kukabiliwa na maswali mazito kutoka pande zote mbili, Barr aliamua kutorudi bungeni siku ya pili kuhojiwa na Tume ya Sheria ya Baraza la Wawakilishi linalodhibitiwa na wapinzani, Wademokrats.

Kutokana na hatua hiyo Mwanasheria Mkuu huyo alikosolewa vikali, na waliomkosoa walidadisi iwapo yeye ni Mwanasheria Mkuu wa serikali au wakili wa Trump.

Wademokrats nao wanatishia kupiga kura wiki ijayo ya kumfungulia mashtaka Mwanasheria Mkuu kwa kukaidi amri, akiendelea na msimamo wake wa kukataa kwenda bungeni kusikilizwa, na hasa ikiwa hatowasilisha ripoti kamili ya Mwendesha Mashtaka maalum Robert Muller kuhusiana na uchunguzi juu ya Rashia kuhusika kuingilia kati uchaguzi mkuu Marekani wa 2016.

Barr anadai ripoti hiyo imeondoa tuhuma zote dhidi ya kampeni ya rais Trump na yeye mwenyewe kuhusiana na njama hiyo ya Rashia.

Lakini Mueller na Wademokrats pamoja na ripoti wanathibitisha kulikuwepo na ushirikiano kati ya Rashia na kampeni ya Trump. Lakini Mueller alieleza kwamba hakuweza kutoa uamuzi wa mwisho kwani hilo ni jukumu la Bunge na hasa kwa vile Wizara ya Sheria ilitoa kanuni inayosema rais aliyeko madarakani hawezi kufunguliwa mashtaka.

White House na Barr wakiendelea kukaidi amri ya bunge Wademokrat watalazimika kutekeleza jukumu lao la kisheria na kufikisha malalamiko yao mbele ya mahakama. Kwani Katiba ya Marekani imeweka wazi kuwa Bunge linajukumu la kukaguwa na kufuatilia kisheria kazi za serikali. Huu ni mtihani mkubwa unaovikabili vyombo vya utawala vya Marekani baada ya miongo mingi.

Mbali na mvutano huo Wademokrats wamegawika juu ya suala la kumfungulia mashtaka rais au la, kwani ripoti ya Muller inaeleza bayana kwamba Trump alijaribu kuzuia mkondo wa sharia kufanya kazi yake kwa kujaribu kumfukuza kazi Mueller jambo ambalo maafisa wake wa sheria walikataa kutekeleza. Trump hapo awali alimfukuza mkurugenzi mkuu wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai, FBI, James Comey ambaye alikuwa anafanya uchunguzi juu ya Rashia kuingilia kati uchaguzi wa Marekani.

Hivyo wengi wanaamini rais alikuwa na nia ya kuvunja sheria na jambo hilo ni uhalifu na linastahiki kuzingatiwa na Bunge.

Sasa Wademokrats wamegawika juu ya suala hilo, kwa sababu Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi na wakongwe wa chama hawataki kuanzisha utaratibu wa kumfungulia mashtaka rais wakiwa wamebakiwa na chini ya miaka miwili kabla ya uchaguzi wa Rais wakihisi itaharibu kabisa malengo yao ya kutaka kumtoa kiongozi huyo wakati wa uchaguzi wa 2020.

Wanahisi utaratibu utachukuwa muda, halafu hawatapata nafasi ya kujitayarisha na uchaguzi huo na huenda kitendo chao kikampatia nguvu Trump.

Hata hivyo kwa upande wa vijana chipukizi wa chama cha Demokrats wanataka Rais Trump afuguliwe mashtaka hivi sasa maana wanaamini ametenda uhalifu na inabidi kuwajibika. Lakini changamoto kubwa ni kwamba hata wakimpata na hatia katika Baraza la Wawakilishi , baraza la Seneti linalodhibitiwa na Warepublikan wa chama cha rais hawatafanikiwa kupata theluthi mbili za kura na hivyo kushindwa kumhukumu na atachukua ushindi huo wa kushindwa kuondolewa madarakani na katika kampeni zake.

Hivyo basi nani atakaye kuwa na nguvu kutengua kitendawili hicho cha Washington? wachambuzi wanasema, huu ni wakati wa kipekee wa kisiasa hapa Marekani na hivyo wanawaachia mafahali wawili wapambane na uamuzi utakuwa wa wananchi ambao hawatakubali kuumia, kama wanavyosema wahenga.

Na kama kwamba mvutano huo haujatosha, White House imekabiliwa na mizozo miwili muhimu ya kimataifa.

Ghasia na mapambano yanayoendelea Venezuela kati ya utawala wa Rais Nicolas Maduro na upinzani ukiongozwa na Juan Guaido, Spika wa Bunge aliyejitangaza urais wa muda.

Kiongozi huyo wa upinzani kufikia mwisho wa wiki ameshindwa kuwa rai wanajeshi kuaasi na kumondoa madarakani Maduro, baada ya kuanza kwa wiki kuwepo na mapambano kati ya waandamanaji na wanajeshi pale Guaido alipoonekana na baadhi ya wakuu wa jeshi na kupelekea uvumi wa mapinduzi.

Hali ya sintofahamu ilijitokeza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo kutuliza mambo pale alipokiambia kituo cha televisheni cha CNN kwamba kulikuwepo na ndege iliyokuwa inamsubiri Maduro kuelekea Cuba, lakini Rashia ilimshauri kubaki.

Baadae Maduro kwa ukali alijitokeza na kueleza kwamba Pompeo amesema uongo na hakuwa na nia ya kuondoka.

Baada ya hapo Guaido alitoa wito kwa watu kuandamana kote nchini kuelekea kambi za kijeshi kuwataka wanajeshi waungane nao kuleta mabadiliko lakini badala yake walikabliwa na mabomu ya kutowa machozi.

Bado vyombo vya habari vinafuatilia kuona hali inavyobadilika huko Venezuela. Na hatimae mzozo wa pili ni Korea kaskazini ambako inaripotiwa Kim Jong un amesimamia ufatuaji wa makombora ya masafa mafupi ikiwa ni mara ya kwanza tangu Trump kuingia madarakani miaka miwili ilyopita na Trump kuandika kwenye Twitter kwamba wako pamoja.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG