Mwanadiplomasia huyo, William Taylor, ameeleza mazungumzo ya huko siku za nyuma yaliyokuwa hayajatolewa hadharani yaliosikika na mfanyakazi msaidizi Julai 26, siku moja baada ya Trump kumtaka Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kuchunguza shughuli za kampuni ya gesi asilia Burisma inayomilikiwa na Biden, na mtoto wake Hunter Biden. Na pia kuanzisha nadharia kwamba Ukraine na siyo Russia ilijihusisha na kuvuruga kampeni ya Trump ya 2016 akiwania kuingia White House.
Taylor amesema msaidizi huyo alisikia mazungumzo hayo yaliyokuwa yanajiri kati ya Trump na Gordon Sondland, mchangiaji wa dola milioni moja kwa ajili ya shughuli za siasa za Trump ambaye rais alimteua kuwa balozi Umoja wa Ulaya.
“Mmoja wa wafanyakazi wangu aliweza kumsikia Rais Trump katika simu, akimuuliza Balozi Sondland juu ya uchunguzi,” Taylor ametoa ushahidi. “Balozi Sondland alimwambia Rais Trump kwamba wananchi wa Ukraine walikuwa wako tayari kutekeleza hilo.”
Taylor alisema mazungumzo hayo yaliyosikika yanaonyesha kuwa wakati huo, Trump alijali “zaidi uchunguzi kuliko msaada wa kijeshi wa Ukraine. Taylor alisema Sondland alimwambia “kila kitu” --- msaada wa kijeshi na Zelenskiy akiwa na hamu ya kumzuru Trump White House – itategemea iwapo Ukraine itafungua uchunguzi huo.
Taylor alisema katika kipindi kirefu cha utumishi wake wa diplomasia, hajawahi kamwe kushuhudia rais wa Marekani akiitaka serikali ya nchi nyingine kutekeleza uchunguzi wa kisiasa kujinufaisha yeye binafsi.
Wote wawili yeye na George Kent, afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje anayesimamia uhusiano wa Marekani na Ukraine, walitoa ushahidi kuwa hawakuwa na mawasiliano yoyote na Trump katika kipindi cha miezi kadhaa wakati sakata hilo la Ukraine likitokea.