Mtoa siri wa pili ambae anadai nae pia alisikia mawasiliano ya simu kati ya Rais Trump na Rais wa Ukraine Zelensky amejitokeza, na hivyo kuongeza joto kwenye mjadala kuhusu uchunguzi wa kumuondoa madarakani rais Trump.
Wademocrat katika baraza la waakilishi wanaangazia mawasiliano ya simu kati ya Rais Trump na Rais wa Ukraine, yanayoripotiwa kuwa yalitaka Ukraine kuchafua sifa za mpinzani wake wa kisiasa, mgombea wa tiketi ya urais kutoka chama cha Democrat, Joe Biden.
Trump anasisitiza kwamba hajafanya kosa lolote, akisema kuwa mawasiliano yake ya simu na Rais wa Ukraine yalikuwa mazuri sana. Hata hivyo, wataalam wa sheria wanasema madai dhidi ya Trump yana uzito mkubwa.
Mzozo wa kumfungulia mashtaka Trump umeanza kuzua hisia kali kumhusu Trump kati ya wafuasi na wapinzani wake na huenda ikaharibu zaidi hali ya mgawanyiko wa kisiasa ambao tayari unashuhudiwa nchini.
Wakati huohuo, viongozi wa safa za mbele kutoka chama cha warepublican wanaendelea kumuunga mkono Rais Trump katika sakata hilo.