Trump alitoa tangazo hilo akiwa na Acosta hivi leo Ijumaa nje ya White House kabla ya rais kuanza ziara yake ya majimbo ya magharibi kati ya Wisconsin na Ohio. ‘Nasikitika sana kuliona jambo hili likitokea,’ rais amesema.
“Aliingia makubaliano ya nje ya mahakama ambayo watu waliyapenda. Miaka 12 baadaye, hawafurahishwi nayo tena,” Trump amesema akizungumzia hatua ya Acosta aliyoichukua zaidi ya muongo mmoja uliopita kama mwendesha mashtaka wa serikali kuu, katika kukubali adhabu nyepesi ya kifungo kwa tajiri mkubwa Jeffrey Epstein, ambaye alishutumiwa katika kesi inayohusu usafirishaji haramu wa watoto kwa ajili ya ngono.
“Mtafahamu yote hayo. Ukweli ni kwamba alikuwa waziri mzuri wa kazi,’ amesema rais.
Acosta aliwaambia wana habari kuwa amefanya uamuzi ya kuachia madaraka. ‘Niliongea na rais asubuhi na kumueleza kwamba nadhani itakuwa ni jambo sahihi kwangu mimi kujiweka kando,’ amesema na kuongeza kuwa itakuwa ni ‘ubinafsi’ kubaki katika wadhifa huo, na kuvuruga kile ambacho amekiita ‘ hali nzuri ya kiuchumi tuliyonayo hivi sasa.”
Trump amesema naibu waziri wa kazi, Patrick Pizzella atakaimu kwa muda nafasi ya Acosta, ambaye kujiuzulu kwake kunaanza rasmi katika muda wa siku saba.
Kujiuzulu kwa Acosta kumekuja siku mbili tu baada ya kutetea hatua yake katika kesi ya Epstein.
‘’Bila ya kazi yetu kubwa waendesha mashtaka, Epstein angeweza kutoka kirahisi, na kupewa adhabu ndogo, ambayo ingemfanya aepuke kwenda jela, Acosta aliwaambia waandishi wa habari Jumatao. ‘ “tulifanya kitu ambacho kilihakikisha kuwa Epstein anatumikia kifungo,” amesema.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Khadija Riyami, Washington, DC.