Mwanasheria mkuu wa Marekani, Jeff Sessions,Alhamisi alitangaza kutojihusiha na upelelezi wowote kuhusiana na tuhuma zinazoikabili Russia wakati wa uchaguzi wa rais wa Marekani, mwaka 2016.
Sessions ametangaza hatua hiyo alipokutana na waandishi wa habari mjini Washington DC, baada ya gazeti la Washington Post kuripoti kuwa Sessions, ambaye alikuwa Seneta na mwanachama wa kampeni ya Donald Trump, alifanya mikutano miwili na balozi wa Russia nchini Marekani, Sergei Kislyak, lakini akakosa kutoa habari hizo wakati wa kikao cha kuidhinishwa kwake kama mwanasheria mkuu.
Maswali yalikuwa yameibuka kuhusu iwapo Sessions aljadili maswala yaliyohusu kampeni na balozi huyo. Baadhi ya wajumbe katika bunge la Marekani walimshinikiza kujiondoa kwa uchunguzi huo, huku wakosoaji wake wa mrengo wa Demokratik, wakimtaka kujiuzulu wadhifa wake kama mwanasheria mkuu, wakisema kuwa alisema uongo akiwa chini ya kiapo.
Sessions hata hivyo aliwaambia wanahabari kuwa hakuwa na nia ya kutaka kumpotosha yeyote, na kwamba alitoa majibu kuhusu swala hilo, kulingana na jinsi alivyolielewa swali aliloulizwa na seneta mdemokrat, Al Franken wa Minnesota.