Mexico ilionya Jumatatu kwamba kitisho cha Rais Donald Trump wa Marekani kuiwekea Mexico ushuru mpya wa bidhaa zake zinazosafirishwa kwenda Marekani utaumiza uchumi wa nchi zote mbili na kusababisha wahamiaji zaidi wa Amerika ya kati kusafiri kupitia Mexico ili kufika Marekani.
Kwenye mazungumzo yaliyoanza Washington maafisa wa Mexico walieleza wataweza kufikia kiwango fulani tu cha kutekeleza matakwa ya Trump ya kuzuia mmiminiko wa wahamiaji wanaopitia Mexico ili kuepuka ushuru wa asilimia tano unaotarajiwa kuanza Juni 10.
Maafisa hao walipinga uwezekano wowote wa makubaliano ya nchi ya tatu itakayo walazimu wanaotafuta uhamiaji Marekani kwanza kuomba hifadhi Mexico. Balozi wa Mexico nchini Marekani, Martha Barcena alieleza kwamba kuna kiwango cha juu kabisa watakachoweza kufikia katika majadiliano na kiwango hicho ni hadhi ya Mexico.
Alisema ushuru huo wa Marekani unaweza kusababisha msukosuko wa kifedha na kiuchumi na hivyo kupunguza uwezo wa Marekani kukabiliana na mmiminiko wa wahamiaji.