Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 10:41

Tanzia: Hayati Ali Hassan Mwinyi Muasisi wa Demokrasia na Soko Huria Tanzania


Marehemu Ali Hassan Mwinyi. Picha ya AFP
Marehemu Ali Hassan Mwinyi. Picha ya AFP

Ali Hassan Mwinyi, ambaye katika awamu mbili kama rais wa Tanzania alisimamia kuanzishwa kwa demokrasia ya vyama vingi na kuanzishwa kwa uchumi huria, amefariki akiwa na umri wa miaka 98.

Alizaliwa Mei 8, 1925 katika kijiji cha Kivure katika mkoa wa Pwani. Mwinyi alikulia katika kisiwa kilichokuwa na utawala wa kiasi cha Zanzibar na kufanya kazi ya ualimu kabla ya kujiunga na utumishi wa serikali. Alishikilia nyadhifa mbali mbali za juu, ikiwemo katibu mkuu katika wizara ya elimu ya Zanzibar.

Mwinyi amefariki kutokana na saratani ya mapafu katika mji wa wa kibiashara, Dar es Salaam, nchini Tanzania ambako alikuwa amelazwa hospitali kwa wiki kadhaa, Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza katika kituo cha televisheni cha taifa TBC1.

Rais Tanzania Samia Suluhu . Picha na AFP.
Rais Tanzania Samia Suluhu . Picha na AFP.

Rais Samia ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa, Mwinyi atazikwa Machi 2 huko Zanzibar.

Mwinyi alichukua madaraka mwaka 1985, akimrithi rais aliyeasisi taifa la Tanzania, Julius Nyerere, ambaye aliiongoza nchi hiyo hadi kupata uhuru kutoka kwa utawala wa Kiingereza mwaka 1961 na kuiongoza nchi yenye mfumo wa chama kimoja kwa miaka 24.

Nyerere alianzisha mfumo wa ujamaa wa nyumbani, ambao uliathiri vibaya sana uchumi na kupelekea kusababisha uhaba wa chakula, nguo, mafuta na mahitaji mengine muhimu.

Matatizo haya yaliongezwa na vita vya miezi tisa na nchi jirani ya Uganda vilivyopelekea kupinduliwa kwa dikteta Idi Amin.

Akiwa rais, Mwinyi alilegeza udhibiti wa serikali, akihamasisha uwekezaji binafsi na kufungua uhuru wa vyombo vya habari ambavyo awali vilikuwa chini ya udhibiti wa serikali.

Pia aliboresha uhusiano wa Tanzania na Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Fedha, ambayo yalikuwa na msuguano wakati wa utawala wa Nyerere.

Mfumo wa vyama vingi ulianzishwa mwaka 1992, Mwinyi aliachia madaraka miaka mitatu baadae – akiweka mfano wa kuigwa wa viongozi wa Tanzania kuheshimu ukomo wa muda wa uongozi.

Alisifiwa kimataifa, lakini alivumilia ukosoaji wa hadharani kutoka kwa Nyerere – ambaye alikuwa akiheshimiwa kote kama baba wa taifa – kwa kuachana na siasa ya ujamaa na kushindwa kukabiliana na ufisadi.

Nchini Tanzania Tundu Lissu, mwanasiasa na mwanaharakati maarufu amesisitiza umuhimu wa Mwinyi katika kuimarisha mfumo wa vyama vingi.

Tundu Lissu
Tundu Lissu

"Mzee Mwinyi alileta mabadiliko muhimu katika siasa za Tanzania kwa kuwezesha mazingira ambayo wananchi wanaweza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kisiasa," alisema Lissu.

Rais Mwinyi pia atakumbukwa kwa uwajibikaji pale alipokuwa Waziri katika Wizara ya Mambo ya Ndani mwaka 1976. Wakati huo, alionyesha ujasiri na uwajibikaji kwa kujiuzulu kwa hiari katika nafasi ya uwaziri kama hatua ya kuwajibika kufuatia changamoto zilizojitokeza.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mussa Azan ‘Zungu’ ameelezea jinsi Mwinyi alivyochukua maamuzi hayo.

“Kuna baadhi ya wafungwa walifariki katika gereza la Shinyanga, akachukua jukumu la kujiuzulu baada ya tukio hilo, kwa kuona limemuaibisha kama waziri mwenye dhamana ya mambo ya ndani, akaamua kumuomba Mwalimu Nyerere amkubalie kujiuzulu” amesema Zungu.

Mzee Mwinyi pia ameacha athari chanya katika uchumi wa Tanzania, akiendeleza mageuzi ya kiuchumi na kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali. Kupitia uongozi wake, alitilia mkazo ushirikiano wa kimataifa na kukuza mazingira wezeshi kwa uwekezaji na biashara.

Mzee Ali Hassan Mwinyi alipata sifa ya kutambulika kama "Mzee wa Ruksa" kutokana na tabia yake ya kuwa mtu wa kutoa ruhusa na kutoa fursa kwa watu kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali.

Jina hili lilianza kuenea kutokana na utayari wake wa kutoa idhini au ruksa kwa mambo mbalimbali, iwe ni kwenye masuala ya kisiasa, kiuchumi, au hata katika maisha ya kila siku ya wananchi.

Dr. Wilbrod Slaa
Dr. Wilbrod Slaa

Mwanasiasa mkongwe Wilbrod Peter Slaa anasema, “Mzee Mwinyi alipokuja na sera yake ya kufungua madirisha na milango, basi kila upepo uliingia vizuri na tukapata nafuu tofauti na ilivyokuwa kabla, ambapo hata dawa ya mswaki ilikuwa ngumu kuipata. Kiukweli, aliingia kipindi kigumu, akafanya kazi na Watanzania hawatamsahau kwa hilo, na ndio maana wanamuita mzee ruksa.”

Akirejea katika uwanja wa siasa, Mwinyi alitangazwa kuwa rais wa Zanzibar na makamu wa Rais wa Tanzania mwaka 1984. Baadaye aliteuliwa kuwania urais wa Tanzania mwaka uliofuatia baada ya Nyerere kustaafu.

Mwinyi aliendelea kuishi na familia yake katika mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam baada ya kustaafu urais na kuishi maisha ya kawaida.

Muislam wa kawaida, alikuwa na wake wawili na watoto kadhaa, akiwemo Hussein Mwinyi, rais wa sasa wa Zanzibar.

Baadhi ya Taarifa katika habari hii inatokana na shirika la habari la Bloomberg na imechangiwa na mwandishi wa VOA Amri Ramadhani

Forum

XS
SM
MD
LG